VIONGOZI WASTAAFU: Mipango mingi ya Waafrika hukwamishwa

Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki akizungumza wakati wa kongamano la viongozi wa Afrika lililoandaliwa na Taasisi ya Uongozi jijini Dar es Salaam jana. Katikati ni Rais mstaafu, Benjamin Mkapa na kulia ni Rais mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo. Picha na Salim Shao
Muktasari:
- Pia yadaiwa baadhi ya viongozi hawatekelezi mambo yanayoamuliwa
Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mstaafu, Cleopa Msuya amesema baadhi ya mipango ya Waafrika imekuwa ikikwamishwa kwenye mikutano ya kimataifa kwa kushindwa kupewa kipaumbele kama ilivyokuwa ikitarajiwa.
Akizungumza jana katika Kongamano la Viongozi wa Afrika lililofanyika jijini hapa, Msuya alisema pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na viongozi wa Afrika kwenye jumuiya za kimataifa, bado ushauri wao umekuwa ukipuuzwa.
Akitoa mfano, Msuya alisema alipokuwa Waziri wa Fedha, aliwahi kuhudhuria mkutano mmoja wa kimataifa ambao yeye na viongozi wengine wa Afrika walitoa mapendekezo yaliyolenga kuleta maendeleo Afrika, lakini hayakufanyiwa kazi.
Alisema mambo mengi yenye manufaa kwa Afrika huzungumzwa katika mikutano hiyo, lakini baada ya kutoka kwenye vyumba vya mikutano ‘wakubwa’ huishia kuzungumza na vyombo vya habari na kuacha hapohapo bila utekelezaji.
Alipendekeza ili kukabiliana na changamoto hizo, viongozi wa Afrika wanaokwenda huko lazima wajiandae kiasi cha kutosha huku wakiwa na sera zinazokubaliana na mipango ya jumuiya za kimataifa.
Akizungumza katika kongamano hilo lililoandaliwa na Uongozi Institute, Rais Mstaafu wa Botswana, Festus Mogae alisema kutokana na changamoto wanazozipata viongozi wa Afrika wanapokuwa kwenye mikutano ya kimataifa, wakati mwingine hulazimika kuandaa risala moja ili kutoa sauti yenye nguvu.
Kwa upande wake, Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa alisema haitoshi kuendelea kuwanyooshea vidole viongozi wao kwa makosa waliyofanya, badala yake waanze kuwasaidia kwa kutoa mbinu mbadala zitakazopunguza changamoto zilizopo.
“Haitoshi kusema viongozi wana upeo mdogo, nataka mapendekezo yanayosema namna ya kutatua matatizo,” alisema Mkapa.
Rais Mstaafu wa Nigeria, Olusegun Obasanjo alisema Afrika imetumia njia moja ya kutafuta maendeleo kwa muda mrefu, kwa hiyo sasa inahitaji itumie njia nyingine kwa kuwa za awali zimeshindwa. Alisema kama wananchi wanaona viongozi wao wanashindwa kutimiza mambo wanayoyataka, watumie njia za kuwashawishi huku akiwaonya kutokutumia nguvu katika kutimiza malengo yao.
Rais Mstaafu wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki alisema pamoja na changamoto za kuleta maendeleo zilizowakabili viongozi wa Afrika, pia wameshindwa kutatua migogoro ambayo imesababisha kutokuwapo kwa amani katika baadhi ya nchi na hivyo kusababisha ongezeko la umaskini kwa watu wake.
“Wakati mwingine utambulisho wa Waafrika umetumika katika namna ambayo umeleta matatizo zaidi hasa tunapozungumzia ukabila, udini na matabaka mengine,” alisema Mbeki.
Mkurugenzi wa Mwalimu Nyerere Foundation, Joseph Butiku alisema viongozi wengi wa Afrika wanafanya mikutano mbalimbali ya kimaendeleo, lakini hakuna bodi inayohakikisha kuwa malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
“Hapa Tanzania nani anasimamia utekelezwaji wa mipango iliyowekwa?” alihoji Butiku.