Vipindi vya sikukuu, Januari  ya ada, polisi huwa moto

Muktasari:

Kwa Rais Samia, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na IGP Camillus Wambura, Jeshi la Polisi linahitaji usafi mkubwa. Moja ya alama za taifa lililokufa kimaadili ni walinzi wake wa amani na usalama kugeuka wahalifu.

Maofisa saba wa polisi wanashtakiwa kwa kumuua mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis, baada ya kudaiwa kumpora fedha zake. Ni kesi namba 15/2023, Mahakama Kuu, Mtwara.

Mussa alikamatwa kama mtuhumiwa, akawekwa mahabusu Kituo cha Mitengo, Mtwara. Inadaiwa maofisa hao walimchoma sindano ya usingizi, kisha wakamziba mdomo na pua kwa tambala. Mussa alifariki dunia kwa kushindwa kupumua. Ni tukio la Januari 5, 2022.

Christopher Bageni, ambaye alikuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID), Kinondoni, alihukumiwa kunyongwa Septemba 16, 2016. Alikutwa na hatia ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini na dereva teksi mmoja.

Savings Chigumbi, Ephraim Chigumbi na Mathias Lunkombe, walikuwa wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge Morogoro. Pamoja na dereva taksi wa Manzese, Juma Ndugu, walipigwa risasi na polisi na kuuawa, Januari 14, 2006.

Sababu ya kuuawa ni jasho lao, fedha na madini yao. Waliporwa, wakapewa kesi ya ujambazi, kisha wakauawa kwa risasi kwa kisingizio kwamba walikuwa majambazi. Wauaji walikuwa polisi. Walinda amani na usalama.


Bageni, maofisa wengine 12 wa polisi, akiwemo aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Dar es Salaam, Abdallah Zombe, walifikishwa mahakamani kujibu mashitaka ya mauaji na uporaji. Bageni pekee ndiye alikutwa na hatia, akahukumiwa kunyongwa.


Kutoka Januari 2006 mpaka Januari 2022, polisi ni walewale, tabia ni zilezile. Polisi wasijue una fedha. Watakutamani. Watakupa kesi, halafu wanachukua fedha au mali ya thamani uliyonayo.


Mussa na wafanyabiashara wa Mahenge, mazingira ya vifo vyao yanafanana. Wote ni watu wa madini. Wakapewa kesi, wakaharakishiwa umauti, lengo kuu likiwa kupora fedha na madini yao.


Wote waliuawa kama wahalifu. Kelele za wananchi zikatikisa Ikulu. Rais wa Nne, Jakaya Kikwete, aliunda tume kuchungua mauaji ya wafanyabiashara wa Mahenge. Rais Samia Suluhu Hassan, alimwagiza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuunda kamati kuchunguza mauaji ya Mussa Mtwara.


Tume iliyoundwa na Kikwete, iliyoongozwa na Jaji Mussa Kipenka, iliwasilisha ripoti iliyoonesha kuwa maofisa wa polisi 15 walitenda uhalifu mkubwa. Kamati ya watu tisa iliyoundwa na Majaliwa, iliwabaini maofisa wa polisi saba kuhusika na mauaji ya Mussa.


Polisi na uhalifu


Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa, katika kitabu cha simulizi ya maisha yake, alichokipa jina; “My Life, My Purpose” – “Maisha Yangu, Kusudi Langu”, ndani yake anasimulia kuhusu maofisa wa polisi wa usalama barabarani, trafiki.


Mkapa ameandika kuwa alipokuwa rais, alipita barabarani na kuona maeneo mengi Dar es Salaam kuna makundi ya trafiki. Aliwauliza wasaidizi wake sababu ya trafiki kujazana vile barabarani. Alijibiwa: “Sikukuu.”


Ndiyo, Mkapa alijulishwa kuwa trafiki hujazana barabarani inapokaribia vipindi vya sikukuu ili kuchukua rushwa. Fedha za kustarehesha familia vipindi vya sikukuu, husakwa na trafiki kwa rushwa za kulazimisha.


Mkapa alisema, hata baada ya yeye kuondoka madarakani, alishangaa akipita barabarani vipindi vya kukaribia sikukuu, hali iliendelea hivyohivyo. Angalau suala la trafiki na makusanyo ya sikukuu barabarani, limesemwa na mmoja wa viongozi wa juu kabisa Tanzania.


Kutoka Novemba 12, 2019, Mkapa alipozindua kitabu “My Life, My Purpose”, kisha Julai 24, 2020, Mkapa alipofiriki dunia, hadi sasa, Tanzania haijabadilika. Hali ni ileile, mambo ni yaleyale, trafiki wapo vilevile. Siku hizi wana msemo wao kwamba “wanasaka maokoto”.


Kama Rais alilijua, bila shaka wakuu wa polisi (ma-IGP), wa vipindi mbalimbali, wanajua hiyo tabia ya trafiki. Mawaziri wa Mambo ya Ndani (Usalama), wanafahamu hicho kitu. Swali je, mbona tabia hiyo haikomi? Imehalalishwa?


Angalau Rais wa Tano, Dk John Magufuli, yeye alitamka hadharani kuwa “trafiki kupewa Sh5,000 ya kung’arisha viatu hakuna ubaya.” Rais alihalalisha rushwa waziwazi, wakati sheria zipo wazi kwamba kitendo hicho ni jinai.


Matawi ya uhalifu


Kwa mujibu wa mchanganuo wa uhalifu wa polisi, yapo makundi matatu. Mawili yana sura inayozoeleka ya rushwa, moja ni uhalifu wa mipango (organized crime).


Mosi, inaitwa “solicit”, yaani nipe nikupe. Polisi wanachukua rushwa ili kuyafumbia macho makosa. Kama trafiki barabarani, wanavuta mlungula na kuacha magari yaliyovunja sheria za barabarani yakitembea bila kuripotiwa.


Pili, upendeleo wa aina ya watu wa kuwaadhibu, inaitwa “selective enforcement”. Watu wawili wanafanya kosa moja, mwingine anaadhibiwa, mwenzake anaachwa pasipo haki.


Tatu, inaitwa “flouting”, yaani uharamia wa kubambikia watu kesi pamoja na uhalifu wa mipango. Hapa ndipo kesi za wafanyabiashara wa madini waliouawa, zinapoingia kwenye muktadha.


Hata rushwa za trafiki vipindi vya sikukuu, hutakosea ukiiweka kwenye uhalifu wa mipango. Makundi ya askari wenye sare nyeupe na khaki, wanawake weupe kwa bluu, wanavizia magari kwa presha kubwa kutafuta “maokoto”.


Gari linasimamishwa dakika 10, linakaguliwa. Makosa ya kutafuta. “kanyaga breki”, “washa taa”, “piga honi”, hadi wipers zinakaguliwa kipindi cha jua kali. Unakuwa mpango maalum wa kutafuta fedha za sikukuu.


Nimewahi kushuhudia trafiki anamkomalia dereva taksi, anamtishia kumwandikia faini kwa sababu stika ya “nenda kwa usalama barabarani” ilibandikwa kulia. Trafiki akasema kisheria stika inabandikwa kushoto.


Yule dereva akawa analalamika hadi machozi. Nikamuuliza yule trafiki, sheria namba ngapi ya mwaka gani, inayosema stika ikibandikwa kulia kwenye kioo cha gari ni kosa lenye kustahili adhabu? Ukweli, rushwa ilikuwa inatafutwa kwa nguvu.


Trafiki hawataki kabisa kutimiza jukumu la kutoa elimu. Eneo la kutoa maelekezo kwa ajili ya kusaidia usalama barabarani wao wanatazama fedha. Ukitoa rushwa, unalipa kidogo. Usipotoa, utakutana rungu zito la faini.


Sikukuu na ada


Rafiki yangu mwanasheria, mtaalamu wa sheria ya uhalifu (criminal law), aliwahi kuning’ata sikio kuwa matukio mengi ya polisi kuhusishwa kufanya uhalifu mkubwa, hutokea nyakati za msako wa fedha za sikukuu na ada.


Akanikumbusha kuwa wafanyabiashara wa Mahenge waliuawa Januari 2006. Mussa na fedha zake za madini, alitolewa roho Januari 2022. Wote hao waliporwa fedha. Januari ni kipindi cha malipo ya ada za wanafunzi.


Desemba ina hekaheka za matumizi. Likizo familia, fedha za sikukuu, shopping za mavazi, chakula na vinywaji. Januari inafika akaunti zimenuna. Ada za shule zinatakiwa, jumlisha malipo ya pango.


Katikati ya fikra hizo, unawaona trafiki wakiwa wakali barabarani kusaka fedha. Maofisa wa polisi wanaingia kwenye ujambazi wa kupora fedha za raia wema hadi kuwaua. Tafsiri ya kijamii inakuwa ni msako wa fedha za sikukuu, ada na kodi za pango.


Watu ambao wameitikia wito wa jeshi kulinda raia na mali zao. Wakapewa mafunzo kwa gharama za walipa kodi. Wanalipwa mishahara, posho kemkemu, wengine hadi nyumba wanazoishi, fedha zinatoka kwa Watanzania wanaovuja jasho na kulipa kodi.


Kisha, kwa tamaa zao na kwa kutaka kuishi juu ya vipato vyao, wanaamua kuwafanyia ujambazi wavuja jasho wanaowezesha wao kulipwa mishahara, posho na stahiki nyingine wanazopata.


Usafi mkubwa unahitajika


Ujambazi ni sehemu ya jeshi la polisi au kuna majambazi yamejiingiza jeshini?


Vijana wanaojiunga jeshi wanafuzu vigezo vipi? Majeshi huwa na idara za masuala ya ndani, yaani Internal Affairs “IA”. Wajibu wake ni kuchunguza makosa na mienendo ya askari. IA ya Polisi Tanzania ipo hai?


Mwaka 2006 wafanyabiashara wa madini waliuawa. Miaka 16 baadaye mfanyabiashara wa madini anauawa. Nini kilifanyika mauaji ya kwanza yalipotokea ili kudhibiti yasijirudie? Usalama wa nchi ukoje ikiwa polisi ndiyo watuhumiwa wa ujambazi?


Kwa Rais Samia, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni na IGP Camillus Wambura, Jeshi la Polisi linahitaji usafi mkubwa. Moja ya alama za taifa lililokufa kimaadili ni walinzi wake wa amani na usalama kugeuka wahalifu.