Vipodozi, vinywaji vikali, kulipia bima ya afya

New Content Item (2)

Dodoma. Hatimaye Serikali imeuwasilisha bungeni Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa watu wote wa mwaka 2022 ikiainisha vyanzo mbalimbali vya mapato vitakavyogharamia watu wasiojiweza vikiwemo vya vipodozi, vinywaji vikali na michezo ya kubahatisha.

Vingine ni vinywaji vyenye kaboni, mapato yatokanayo na ushuru wa miamala ya kielekroniki kwa kadri itakavyopendekezwa na waziri wa fedha, fedha zitokanazo na Bunge, mapato yatokanayo na uwekezaji wa mfuko na zawadi na misaada kutoka kwa wadau.

Vyanzo hivyo vilibainishwa leo Jumatano Novemba Mosi, 2023 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akiuwasilisha muswada huo uliokwama mara mbili, Novemba mwaka jana na Februari mwaka huu kwa sababu ya kutokuwapo kwa chanzo cha uhakika cha mapato kugharamia kundi hilo.

Waziri Ummy amesema idadi ya watu wanaohudumiwa na bima ni asilimia 15 wakati asilimia 85 wapo nje ya huduma hiyo.

“Takribani asilimia 85 ya Watanzania wapo nje ya utaratibu huo kutokana na utayari wa kujiunga na bima za afya, takwimu zinaonyesha hadi Septemba 2023 ni asilimia 15.3 tu ya wananchi wote ndio wapo katika mfumo wa bima ya afya ambapo asilimia 8 wapo NHIF, asilimia 0.3 ni NSSF-SHIB Bima Binafsi inachukua asilimia 1,” amesema .

Amesema Takwimu za Matumizi ya kaya Binafsi (Household Budget Survey – HBS) kwa mwaka 2017/18 zinaonyesha asilimia 26.4 ya watu wote Tanzania Bara (59,851,347) hawana uwezo ambayo ni watu 15.8 milioni  sawa na kaya 3.6, wananchi wasio na uwezo na ambao wanaishi katika umaskini uliokithiri ni 4.04 milioni ambao ni asiliia 8 sawa na kaya 1,113,513.


Jinsi itakavyoanzishwa

Waziri Ummy amesema Muswada unapendekeza Mfumo wa Bima ya Afya kwa wote ujumuishe waajiri, watumishi wa umma, wafanyakazi walioajiriwa katika sekta binafsi, waliojiajiri wenyewe katika sekta isiyo rasmi na wananchi wasio na uwezo.

“Kufanya hivi kutasaidia kuondoa vikwazo ikiwemo wananchi kutopata huduma za afya wanapokuwa nje ya maeneo waliyojiandikisha ambapo walilazimika kulipia huduma za afya kwa utaratibu wa papo kwa papo,” amesema Waziri Ummy

Amesema kikwazo kingine kilikuwa ni ufinyu wa huduma katika kitita cha mafao kinachotolewa na hivyo kukosekana kwa huduma muhimu mathalani huduma za afya ya kinywa na meno, kutojumuishwa kwa baadhi ya dawa na kumlazimu mwanachama kulipia.

Waziri huyo amesema kingine ni muundo wa Mfuko wa Afya ya Jamii ulioboreshwa (CHF) kutokidhi misingi na kanuni za uendeshaji wa bima ya afya mathalani kutotenganisha kwa majukumu kati ya mnunuzi na mtoa huduma za afya lakini uhiari wa wananchi kujiunga unaosababisha wengi kujiunga wakiwa wagonjwa.

Alisema Serikali ilipendekeza mchango wa asilimia sita wa mshahara utakuwa kwa ajili ya mwajiri wa sekta ya umma na mwajiri wa sekta rasmi binafsi atakayechagua

kuwasajili waajiriwa wake katika skimu ya bima ya afya ya wote wenye lengo la ugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo.

“Wanifaika katika mfuko huo sasa wataweza kugharamia huduma za matibabu kwa magonjwa sugu na ya muda mrefu kama saratani na magonjwa ya figo na huduma za dharura zitokanazo na ajali,” amesema 

Waziri Ummy amesema Serikali inalenga kila mtu nchini awe na bima ya afya ili kuwa na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua.

Ameeleza muswada unalenga kuboreshwa kwa vitita vya mafao vinavyotolewa na skimu za bima ya afya na kuimarisha hali ya kipato kwa wananchi ambako kutapunguza malalamiko ikiwemo maiti kuzuiwa hospitalini kwa kukosa fedha za matibu.

Kwa mujibu wa muswada huo kifungu cha 33 kinazungumzia mamlaka ya kutunga kanuni zitakuwa chini ya waziri mwenye dhamana kuwa; utaratibu wa usajili wa skimu za bima ya afya, kitita cha mafao, muda na masharti au wigo wa kitita cha mafao kwa kushirikiana na mamlaka.

Pia, waziri ataandaa utaratibu wa kuanzisha kitita cha mafao maalum katika skimu ya bima ya afya ya umma, utaratibu wa utambuzi wa watu walio katika sekta isiyo rasmi na namna ya kuwasajilii katika skimu, utaratibu wa kuboresha kitita cha mafao katika skimu ya bima ya afya ya umma na suala lingine lolote kwa ajili ya utekelezaji bora wa masharti ya Sheria hii.