Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vishkwambi kuboresha sekta ya kilimo, Waziri Bashe atoa maelekezo

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Maofisa ugani nchini wamepewa vitendea kazi ili waweze kuwahudumia wakulima kuanzia ngazi ya kijiji.

Dodoma. Serikali ya Tanzania imeshaunda mfumo wa maofisa ugani wa kilimo, mifugo na uvuvi na kuwapatia vitendea kazi ili waweze kuwahudumia wakulima kuanzia ngazi za chini.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Mei 7, 2024 na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwenye uzinduzi wa ugawaji wa vishkwambi 3,500 na Pos mashine kwa maofisa ugani, kilimo na mawakala wa pembejeo za kilimo jijini Dodoma.

Bashe amesema kwa sasa wanaanza programu ya ujenzi wa nyumba za maofisa ugani kwenye kata na vijiji, ambapo fedha za ujenzi wake  zitatumwa kwenye halmashauri itakayosimamia ujenzi ambapo zimeshatumwa  fedha za kujenga nyumba 50 za kwanza.

“Lengo letu ni tunapojenga skimu ya umwagiliaji mkandarasi ni lazima ajenge nyumba ya ofisa ugani kwa hiyo njia ya kwanza ya kupata nyumba za maofisa ugani, lakini pia kutoka kwenye bajeti tutakuwa tunatenga fedha za kujenga nyumba hizo ili  wakakae kulekule vijijini ambako wakulima wapo,” amesema Bashe.

Amesema kwa kutumia mfumo wa maofisa ugani wanataka wakuu wa mikoa na maofisa tawala wa mikoa wawe na uwezo wa kuona kila kitu kinachofanywa na maofisa hao, hasa idadi ya wakulima waliotembelewa na kupewa elimu.

Bashe amesema, “mpaka sasa Serikali imeshapeleka vifaa vya kupimia udongo kwenye halmashauri 142 ambayo ni huduma ya bure kwa mkulima ili aweze kupata taarifa za afya ya udongo iliyopo shambani kwake ambayo itamweleza ni aina gani ya mazao anayotakiwa kulima kulingana na taarifa ya udongo iliyopo.

Mbali na hilo, Waziri Bashe amesema wameshusha mradi Jenga Kesho Iliyo bora (BBT) kwenye ngazi ya halmashauri na mikoa ambapo mwongozo wake utazinduliwa na kutumwa kwa wakuu wa mikoa.

“Sisi tunachokitaka ni nyinyi muamue tu hekta 200 ziko hapa sisi kama wizara tunachokileta ni uwekezaji wa kujenga miundombinu ya umwagiliaji ili shughuli ya uzalishaji iendelee,” amesema Bashe.

Amesema uchaguzi wa vijana utafanyika kwenye ngazi ya mikoa wakishatambuliwa watapewa mafunzo kwenye vituo vya wizara ya kilimo vilivyopo kwenye kanda zote nchini, ambapo wizara itasimamia suala la mafunzo ili mradi wao ndiyo waseme huyu ni mkulima.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Charles Mahera amesema ofisi hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo na wadau wengine, ili kuwezesha wakulima kuongeza tija na kuimarisha mnyororo wa thamani.

“Na mimi nimeshawahi kuwa Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya kuna watu wengine huko wanakuwa kama wapo likizo msipojua wanakuwa wanafanya mambo yao tu, kwa mfano hao maofisa ugani wapo kwenye ngazi za kata lakini wananchi hawajui kama wapo,” amesema Dk Mahera.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA), Dk Sophia Kashenge amesema uzalishaji wa mbegu bora nchini bado uko chini hali inayotishia usalama wa chakula.

Amesema hiyo inatokana na wakulima wengi kung’ang’ania mbegu za kienyeji ambazo zina ukomo kwenye uzalishaji wake hata kama zikiwekewa mazingira mazuri ya uzalishaji, na kushauri wakulima kuanza kutumia mbegu zilizoboreshwa ambazo zinatoa mazao mengi.