Prime
Vyuo kutumia namba za Nida kupata matibabu

Muktasari:
- Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema wanafunzi wa elimu ya juu nchini wataanza kutumia namba zao za Vitambulisho vya Taifa (Nida) kupata huduma za afya, badala ya kadi ya bima ya afya.
Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesema wanafunzi wa elimu ya juu nchini wataanza kutumia namba zao za Vitambulisho vya Taifa (Nida) kupata huduma za afya, badala ya kadi ya bima ya afya.
Kauli hiyo ni ufafanuzi wa taarifa iliyotolewa na Jumuiya ya Wanafunzi Taasisi ya Elimu ya Juu Tanzania (Tahliso) ikiwataka wanafunzi wote wenye umri kuanzia miaka 18 kuendelea kujisajili kupata vitambulisho vya Nida ambavyo ndivyo vitatumika kama kadi za bima ya afya.
Kwa mujibu wa Tahliso, tayari wanafunzi wa mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma kwa mwaka wa masomo uliopita walianza kutumia Nida kupata huduma za afya na awamu hii utahusisha wanafunzi wote nchini.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Meneja Uhusiano wa NHIF, Angela Mziray amesema kwa sasa mifumo mingi ya Serikali inaunganishwa na Nida ili kusiwe na mwingiliano wa taarifa.
“Tutakapofanikiwa wanafunzi kuwa na namba za Nida, hakuna haja ya kuwatengenezea kitambulisho cha NHIF, akiwa na namba akifika hospitali atachukuliwa alama ya dole gumba, taarifa zake zitaonekana na atathibitishwa kama mwanachama wa NHIF, kwa kuwa kutakuwa na mwingiliano wa mifumo ya Nida na NHIF,” amesema.
Kuhusu hatua zilizoanza kuchukuliwa ili wanafunzi wengi kuwa na namba ya Nida, Kamishna wa Afya na Mazingira wa Tahliso, Christian Kimaro alisema wameanza kutoa elimu kwa wanafunzi, hasa mikoa yenye vyuo vingi.
Arusha na Mwanza ni miongoni mwa mikoa aliyoitaja akieleza kuwa tayari wamefanya mazungumzo na NHIF na Nida ili kuangalia namna ya kuvifikia vyuo wakati wa usajili.
“Tutaorodhesha majina yote ya wanafunzi wasio na namba za Nida ili wapate, watu wafahamu kitakachokwenda kutumika ni namba ya Nida na sio kadi,” amesema.
Kuhusu utambuzi wa mtu kama ni mwanafunzi, Kimaro alisema mwanafunzi anaposajiliwa chuoni taarifa zake huingizwa kwenye kitambulisho cha Nida, hivyo anapokwenda kutafuta huduma taarifa zake zote zitaonekana.
“Pia muonekano wa uso na taarifa za alama za vidole navyo vitatumika kumtambua mhusika kama ni mwanafunzi.
“Faida tutakayoipata wanachuo za kuunganisha mifumo hiyo, ni kuanza kupata huduma pale unapolipia, tofauti na awali ambapo ilikuwa hadi kadi za bima ya afya zinapotolewa,” amesema.
Takwimu za Nida
Kwa mujibu wa Nida, watu milioni 24.1 wamesajiliwa na mamlaka hiyo, huku namba za usajili zilizotolewa zikiwa ni milioni 20.1.
Pia vitambulisho vilivyozalishwa ni milioni 13, kwa mantiki hiyo, takwimu hizo zinaifanya idadi ya watu wenye vitambulisho vya Nida kuwa ni asilimia 67 na asilimia 32 hawajapata.