Waajiri wakumbushia punguzo kodi ya ujuzi

Muktasari:

  • Bado kilio cha waajiri kuhusu Serikali kupunguza kodi ya Maendeleo ya Ujuzi (SDL) kimeendelea kuwepo, wakisisitiza kupunguzwa kwake kutarahisisha ufanyaji biashara.

Dar es Salaam. Licha ya hatua mbalimbali za Serikali kupunguza kodi ya Maendeleo ya Ujuzi (SDL) kutoka asilimia sita hadi 4.5, waajiri wametaka kuendelea kupunguzwa zaidi hadi kufikia asilimia mbili.

Kwa mujibu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), hatua ya kupunguzwa kwa kodi hiyo itarahisisha mazingira ya biashara na kupunguza gharama.

Kodi ya SDL hulipwa na kampuni kwenye mshahara ghafi wa kila mfanyakazi, ambayo kwa sasa imefikia asilimia 4.5.

Hoja ya ATE kuhusu kupunguzwa kwa kodi hiyo, inatokana na ahadi ya Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba katika hotuba yake aliyoitoa kwenye Bunge la bajeti mwaka jana, aliposema Serikali itapunguza kodi hiyo kila mwaka hadi kufikia asilimia mbili.

Kauli hiyo iliibuliwa na Mwenyekiti wa ATE, Oscar Mgaya, leo Mei Mosi, 2024  alipokuwa akizungumza katika sherehe za Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani ‘Mei Mosi’ ambazo kitaifa zinafanyika mkoani Arusha.

Mgaya ametumia jukwaa hilo, kuiomba Serikali itekeleze ahadi yake ya kupunguza kodi hiyo kila mwaka hadi itakapofikia asilimia mbili.

“Ni matumaini yetu kuwa ile ahadi ya Waziri wa Fedha katika hotuba yake ya bajeti ya mwaka jana ataikumbuka na kuendelea kupunguza kodi ya SDL kidogokidogo kila mwaka hadi itakapofika asilimia mbili,” amesema.