Waandamana kupinga kupunguzwa kazini

Muktasari:

Wakizungumza na waandishi wa habari leo mgodini hapo wafanyakazi hao walimuomba Rais Dk John Magufuli kuingilia kati suala hilo kwani wanataka kuonewa na kukosa haki zao za msingi ili hali wamepoteza muda na nguvu zao.

Mirerani. Wafanyakazi wa kampuni ya TanzaniteOne wameandamana kupinga uongozi wa kampuni hiyo kutaka kuwapunguza wafanyakazi 635 bila taratibu za kisheria, kwa madai kuwa wanajiendesha kwa hasara na wao kupoteza haki zao.

 

Wakizungumza na waandishi wa habari leo mgodini hapo wafanyakazi hao walimuomba Rais Dk John Magufuli kuingilia kati suala hilo kwani wanataka kuonewa na kukosa haki zao za msingi ili hali wamepoteza muda na nguvu zao.

 

Mfanyakazi wa mgodi huo, Felician Costerntine alisema kampuni hiyo inaendesha shughuli zake kwa usanii na kushindwa kufanya kazi kitaalamu hivyo iondolewe na kupewa mwekezaji mwingine anayeweza kuendesha migodi hiyo.

 

“Ni bora wakati mzungu wa TanzaniteOne alikuwa anafanya kazi hapa, huyu mzawa wa Sky Group aliponunua hisa, hivi sasa ameshindwa kuiendesha anataka kuachisha watu bila haki Magufuli ingilia kati,” alisema Costerntine.

 

Alisema kampuni hiyo inatakiwa kutekeleza agizo la serikali linalohitaji wafanyakazi wote 1,258 kupatiwa mikataba ya ajira, tangu kampuni hiyo ya Sky Group iliponunua hisa Novemba mwaka jana na kuwalipa stahiki zao zote.

 

Mfanyakazi wa kampuni hiyo Sofia Mbimbi alisema Rais Magufuli kila wakati amekuwa akinadi kauli mbiu ya hapa ni kazi tu hivyo dhana hiyo inatakiwa kuendelezwa kila mahali na siyo kupunguza wafanyakazi wengi wanaoifikia 635.

 

“Maana ya hapa ni kazi tuu ni nini, endapo watu wengi kama hao wanapunguzwa, Magufuli aje hapa kwani hawa wawekezaji wanaendesha mambo bila kufuata sheria na kutaka kupunguza watu ovyo,” alisema Mbimbi.

 

Alisema hivi karibuni kamishna wa madini nchini na mkurugenzi wa Stamico, walitembelea mgodi huo na kudanganywa kuwa kazi zinaendelea vizuri, ila sasa kampuni hiyo inadai inajiendesha kwa hasara na inataka kuwapunguza kazi.

 

Mwishoni mwa wiki iliyopita uongozi wa kampuni hiyo, kampuni ya madini Stamico yenye hisa 50, ulikutana na viongozi wa chama cha wafanyakazi migodini (Tamico) tawi la TanzaniteOne kujadili hilo ila ukakosekana muafaka.

 

Kikao hicho kilishindwa kumalizika na kusababisha suala hilo kufikishwa kwenye kituo cha polisi Mirerani na kufungua jalada lenye namba MER/RB/2820/2015 baada ya mtumishi wa Stamico kuwatolea lugha ya matusi viongozi wa Tamico. 

 

Hata hivyo, Ofisa mwajiri wa kampuni hiyo Kiria Laizer akizungumza kwa njia ya simu jana alithibitisha kuwepo na mchakato wa mpango wa kupunguzwa kazi kwa wafanyakazi 635 wa kampuni hiyo.

 

“Hayo mambo mengine utanisamehe ndugu yangu kwani mimi siwezi kuyajibu ila inatakiwa uwaulize viongozi wa juu kwani mimi siyo msemaji wa kampuni na hivi sasa nataka nikafanye kikao na wafanyakazi,” alisema Laizer.