Waandishi wamkumbusha Waziri Nape ahadi magari ya misafara

Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), Greyson Kakuru akifafanua jambo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyofanyika Mei 18, 2023 mjini Shinyanga. Picha na Suzy Butondo
Muktasari:
Waziri Nape alitoa ahadi hiyo Januari 12, 2022 wakati wa ibada ya kitaifa ya kutoa heshima za mwisho kwa waandishi wa habari watano waliofariki kwa ajali ya gari wakienda kushiriki ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Ibada hiyo ilifanyika viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza.
Shinyanga. Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga, Greyson Kakuru ameikumbusha Serikali ahadi ya ubora wa magari ya waandishi wa habari kwenye misafara ya viongozi baada ya mazoea ya kupewa magari yasiyo na ubora kuendelea.
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari (Media Day) yaliyandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), Kakuru amesema ahadi hiyo iliyotolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye bado haitekelezwi kwa waandishi kuendelea kupangiwa magari mabovu wakati wa ziara za viongozi.
Waziri Nape alitoa ahadi hiyo Januari 12, 2022 katika viwanja vya Nyamagana jijini Mwanza wakati wa ibada ya kitaifa ya kutoa heshima za mwisho kwa waandishi wa habari watano waliofariki kwa ajali ya gari wakienda wilayani Ukerewa kushiriki ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
"Tunaiomba Serikali kutuondolea kadhia hii waandishi wa habari ambao kwa hakika ni sehemu muhimu wakati wa ziara za viongozi kwa sababu ndio tunahabarisha umma yanayojiri na maagizo ya Serikali,’’ amesema Kakuru
Kuhusu upatikanaji wa habari, Mwenyekiti huyo SPC amewasihi viongozi, watendaji na maofisa habari katika mamlaka na taasisi za umma kuacha urasimu wa kutoa taarifa kwa faida ya umma.
Amekemea tabia ya baadhi ya viongozi na watendaji wasiopenda maovu na madhaifu yao kufichuliwa kuwapigia simu wamiliki na wahariri kuwachongea waandishi au kutishia kushtaki pindi habari za uchunguzi zinapoandikwa.
‘’Baadhi ya viongozi na watendaji hawapendi habari za uchunguzi na huwapigia wamiliki na wahariri kutishia kushtaki; huku siyo tu ni kuminya uhuru wa habari, bali pia kutumia vibaya madaraka kuficha udhaifu,’’ amesema Kakuru
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Johari Samizi aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amewataka maofisa habari katika taasisi na mamlaka za Serikali kushirikiana na waandishi wa habari kwa kutoa taarifa zote muhimu zinazohusu utendaji wa Serikali na maendeleo ya wananchi.
Huku akiwapongeza waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga kwa kazi nzuri ya kuhabarisha umma na kuhamasisha maendeleo, Samizi amesema taaluma ya habari ni miongoni mwa taaluma muhimu zinazosaidia siyo tu kufikisha ujumbe, bali pia kuhamasisha jamii katika masuala mbalimbali ikiwemo maendeleo.
“Waandishi wa habari Shinyanga na kote nchini wanafanya kazi nzuri ya kuhabarisha jamii; wito wangu kwao ni kuendelea kutumia vema kalamu zao kwa maslahi na faida ya umma,’’ amesema Samizi.
Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa, Francis Mihayo amewataka watoa huduma za maudhui kuzingatia sheria ikiwemo kupata leseni za kutoa huduma.
“Nawasihi wenye Blogs na Online Tv wahakikishe wanazisajili na kupata leseni huku wakizingatia sheria na kanuni za kitaaluma katika kazi zao,’’ amesema Mihayo