Waanza kupata gawio baada ya kusota kwa miaka 88
Muktasari:
- TFA iliyoanzishwa mwaka 1935 hadi sasa ina jumla ya wanahisa 4,800 wote wakiwa na kilio kikubwa cha kupata faida kutokana na fedha zao walizoziwekeza bila matumaini.
Arusha. Wanahisa wa Chama cha Wakulima Tanganyika (TFA) wanatarajia kuanza kupata gawio la hisa zao walizoziwekeza kwa zaidi ya miaka 88 sasa tangu kuanzishwa kwa umoja huo.
TFA iliyoanzishwa mwaka 1935 hadi sasa ina jumla ya wanahisa 4,800 wote wakiwa na kilio kikubwa cha kupata faida kutokana na fedha zao walizoziwekeza bila matumaini.
Akizungumza jijini Arusha kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa TFA, Mkurugenzi Mtendaji, Justine Shirima amesema kuwa kwa mwaka wa fedha ulioanza Oktoba 2023 hadi 2024 wanachama hao wataanza kupata gawio.
“Miaka mingine kampuni ilishindwa kutoa gawio kutokana na ilikuwa inajiendesha kwa hasara huku gharama za uendeshaji na matumizi yakiwa makubwa kulinganisha na mapato yaliyokuwa yanaingiza,” amesema na kuongeza…
“Kuanzia mwakani wanahisa wa kampuni ya TFA wataanza kunufaika na gawio kutokana kupungua kwa hasara na kuongezeka kwa ufanisi na nidhamu ya matumizi na udhibiti wa gharama za biashara iliyosaidia kuanza kupata faida kwa misimu huu,” amesema.
Amesema kuwa wamefanikiwa kupunguza kiwango cha hasara hadi kufikia Sh1.49 bilioni kwa mwaka 2023 kutoka Sh11.3 bilioni kwa miaka mitatu iliyopita katika vyanzo vyao vya mapato ikiwemo kodi ya mapango, biashara ya pembejeo na mashine mbali mbali wanazomiliki.
Amesema kuwa mtaji umefikia kiasi cha Sh52.1 bilioni kwa thamani ya majengo, mashine na vifaa mbalimbali wanavyomiliki na kufanya ongezeko la Sh4.6 bilioni kutoka Sh47.5 bilioni.
“Kutokana na hayo tumeripoti ongezeko la Sh1.4 bilioni katika biashara ya pembejeo na Sh268 milioni kwenye kodi ya pango, na malengo yetu ni kuimarika kwa faida katika mwaka ujao wa 2023/ 2024, hivyo kwa matumaini hayo wanachama wajue kampuni inaingiza faida na wataanza kupata gawio,” amesema Shirima.
Aidha majibu hayo yametokana na maswali ya wanachama wakiwemo Eugenia Kweka na John Mbaga waliohoji utendaji wa kampuni yao wakidai kuwa hawaoni faida ya hisa zao za umiliki kutokana na hawapati chochote zaidi ya kupewa hesabu za hasara kila mwaka huku viongozi wanaoinga madarakani wakijichotea fedha na kukaa pembeni.
“Hakuna kitu kinauma kama unawekeza mahali jasho lako halafu hakuna unachokiona tunaomba leo viongozi mtupe mwelekeo unaotoa majibu ya hatma ya hisa zetu na kama hazina faida mseme kabisa maana wenzetu wanazidi kufa tulioanza nao,” amesema Eugenia.
Mkurugenzi wa Bodi ya TFA, Waziri Barnabas amesema kuwa katika kuongeza ufanisi zaidi wanatarajia kupanua wigo wa kukuza biashara ili kufikia watu wengi zaidi.
“Katika mpango huo tunatarajia kufungua matawi mapya manne katika mikoa ya Kigoma, Rukwa, Mwanza na Singida kwa mwaka 2024,” amesema.
Stanley Mwandry alitumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kuwapatia kibali cha uwakala wa pembejeo za ruzuku kwa bei nafuu ili kuwasaidia wanachama wao zaidi ya 4,800 na wakulima wengine wanaowazunguka kupata kwa wakati lakini pia bila kuchakachuliwa.