Wabunge waikataa ripoti ya Mto Mara

Muktasari:

  • Wabunge leo Jumanne Aprili 5, 2022 wameikataa ripoti ya uchunguzi wa uchafuzi wa maji na vifo katika mto Mara wakisema ni ya aibu na inaifedhehesha nchi.

  

Dodoma. Wabunge leo Jumanne Aprili 5, 2022 wameikataa ripoti ya uchunguzi wa uchafuzi wa maji na vifo katika mto Mara wakisema ni ya aibu na inaifedhehesha nchi.

Ripoti hiyo ni ile iliyofanya uchunguzi wa uchafuzi wa maji kuwa na rangi nyeusi na kusababisha vifo vya samaki katika mto mara ambayo ilikuwa chini ya Profesa Samweli Mayele na wajumbe wengine 10.

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Seleman Jafo aliunda kamati kuchunguza chanzo cha tatizo hilo lakini baada ya kuwasilishwa kwa wananchi ilizua mjadala karibu kila kona.

Leo, wabunge 18 wote wameipinga ripoti hiyo na kuomba isiwekwe kwenye mtandao maalumu wa serikali kwa kuwa maelezo yake ni ya aibu.

Baada ya kamati hiyo kumaliza kuwasilisha ripoti hiyo mbele ya wabunge, mbunge wa Viti Maalumu Neema Rugangira alifungua pazia la kuchangia na alitaja chanzo cha kuwa na taarifa mbovu ni kwa sababu baadhi ya wajumbe wake wana maslahi binafsi.

Rugangira pia alihoji kama uchunguzi ulikuwa unahusisha mambo ya vyakula, kwa nini Wizara ya Afya na Shirika la Viwango (TBS) hawakushirikishwa.

Mbunge huyo pia amehoji ni kwa nini awali kulikuwa na taarifa za kinyesi  na mikojo ya mifugo kuwa ndiyo chanzo, lakini leo imekuja kusema chanzo ni mvua kubwa.

Mbunge mwingine wa Viti Maalumu, Jeska Kishoa amesema tume hiyo haina jipya na akahoji weledi wa wajumbe wake. Amesema kama wana weledi wamewezaje kuthubutu kuisoma ripoti hiyo aliyoiita mbovu na haina afya mbele ya Bunge.

“Kingine lazima tujue watu wa NEMC ni kwa nini mmeshindwa kuzuia bwawa la maji machafu katika mgodi wa North Mara ambalo sharia inasema lisizidi maji lita 800,000 lakini ninyi mmeruhusu hadi lita 2.5 milioni halafu mnasema vitu ambavyo haviingii akilini,” amesema Kishoa.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Muungano na Mazingira Seleman Jafo amesema kuna mambo mengi ambayo yakisomwa kwenye ripoti yatawapa mwanga wabunge na kuonya lazima wachangie kwa umakini kwani wanaweza kuharibu sifa ya nchi kwa wawekezaji.