Wabunge wakomalia kikokotoo, mwalimu amtwisha zigo Kinana

Muktasari:

  • Mjadala wa kikokotoo umeendelea kuibuka kila mahali. Wabunge wameitaka Serikali ya Tanzania kuchukua hatua huku viongozi wa Chama tawala nchini – Chama cha Mapinduzi (CCM) – nao wakikutana na maswali juu ya suala hilo.

Dodoma/Mara. Wakati Serikali ya Tanzania ikisema imesikia kilio cha kanuni mpya ya kikokotoo cha mafao ya wastaafu, wabunge wameendeleza moto bungeni wakiitaka ichukue hatua za haraka.

Mbali na hayo, Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma kwa upande wake amesema matumizi ya kikokotoo kipya yanakwenda kutengeneza Taifa lenye watumishi wezi.

Wabunge walianza kuwasha moto huo bungeni tangu ilipowasilishwa hotuba ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2024/2025.

Walioanza kuzungumzia hilo Ester Bulaya (Viti Maalumu), Mrisho Gambo (Arusha Mjini), Kasalali Mageni (Sumve) na Florent Kyombo (Nkenge) ambao wote waliitaka Serikali kukaa na wafanyakazi na kuirejesha sheria hiyo bungeni.

Mbunge wa Viti Maalumu anayetokana na vyama vya Wafanyakazi, Jane Jerry yeye ametaka elimu itolewe kwa wafanyakazi, huku Mbunge wa Viti Maalumu, Neema Mwandabila akisema fedha za mkupuo za asilimia 33 kutoka asilimia 25, zinatosha kwa kuwa ni ongezeko la asilimia nane.

Kikokotoo hicho ni matokeo ya makubaliano ya pamoja kati ya Serikali, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).

Mei 26, mwaka 2022 Serikali ilitangaza Kanuni mpya za kikokotoo cha mafao ya mkupuo ambacho ni asilimia 33 kwa kila mifuko ya hifadhi ya jamii.

Tangu kutangazwa kwa kanuni hiyo mpya kikokotoo ambacho kilipungua kwa baadhi ya mifuko ya hifadhi ya jamii kwa asilimia 17, kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wafanyakazi wakitaka kirejee kama kilivyokuwa awali.

Kinachopingwa na wafanyakazi ni kanuni mpya ya kikokotoo ya mafao ya mkupuko kuwa asilimia 33 badala ya asilimia 50 kama ilivyokuwa awali.

Aprili 15, 2024, akihitimisha hoja ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema Serikali imesikia ushauri na kupokea maoni mbalimbali kupitia wadau wakiwemo wabunge.

Alisema wamesikia na kupokea maoni kutoka pia kwa wafanyakazi na vyama vya waajiri na wafanyakazi kuhusu kuboresha mafao kwa wafanyakazi wanaostaafu.

Alisema wataendelea kufanya tathmini kuzingatia sheria za kazi ili wafikie hatua nzuri ambayo haitazua malalamiko mengi.

Kuhusu utoaji elimu ya kanuni za mafao kwa watumishi, Majaliwa alisema Serikali itaendelea kutoa elimu ya uhifadhi wa jamii ikiwemo mafao kwa watumishi kupitia njia mbalimbali.

“Nitumie fursa hii kumtaka Waziri wa Kazi na Ajira asimamie kuongeza wigo wa utoaji wa elimu ya mafao kwa watumishi kwa lengo la kujenga uelewa wa kutosha,”alisema Majaliwa.


Kilio cha Musukuma

Leo Jumatano, Aprili 17, 2024, akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa mwaka 2024/25, Musukuma amesema Watanzania wanaliamini Bunge linaweza kuwasaidia katika kulitatua suala hilo.

Alisema yeye ana mwaka wa nane yumo katika Bunge hilo ambapo kuna vitu vinazungumzwa ndani ya chombo hicho, lakini wabunge wanaona kama vile haviwaumizi wananchi.

“Kwa uelewa wangu kama daktari wa akili, ninaona kuwa tunaenda kutengeneza Taifa la watumishi wezi kwa sababu (wafanyakazi) wanalalamika kila siku suala la kikokotoo. Mimi sijasoma sana lakini nikiangalia mtu anapata asilimia 30 halafu asilimia 70 unamtunzia.

Hii inamaanisha kama mtumishi alikuwa apate mafao ya Sh100 milioni anapata Sh30 milioni, ndio akaanze kujenga kaslop (kajumba) lazima niibe tu kwa sababu najua hela zangu kule sitapewa,” amesema.

Alisema hakiwezi kuwa kilio cha kila siku ni lazima mawaziri wakae chini na kutafakari ili kuona kama wanaweza kurudi katika asilimia 50 iliyokuwa awali ama kuwa na namna nyingine ya kuwasaidia wastaafu.

Musukuma alisema haiwezekani Watanzania waendelee kulia na wabunge walizungumzie jambo hilo kwa miaka mitatu mfululizo bila kupatiwa ufumbuzi.

Amesema kama kuna tatizo katika jambo hilo ni vyema watumishi waambiwe la sivyo hakuna mtumishi atakayekuwa mwaminifu.

“Watoto wangu wamemaliza shahada ya kwanza, natakiwa nistaafu, ninatakiwa nikajitegemee, sina nyumba niko katika nyumba ya Serikali halafu naenda kupata asilimia 30 tu (ya mafao yake), lazima niondoke na mzigo liwalo na liwe,” amesema.

Ametaka viongozi wa Serikali kuwekea pamba masikioni bali waone namna ya kuwasikiliza wafanyakazi na kama kuna uwezekano wa kulitatua basi wafanye hivyo.

Musukuma amesema hivi sasa wakisimama kwenye majukwaa ya kisiasa, hakuna watu wanaozungumzia barabara tena ,bali wanazungumzia kuhusu kikokotoo.

“Sisi kama Bunge tuishauri Serikali. Tuone namna ya kutengeneza furaha ya wanaostaafu na wanaokaribia kustaafu na wale wengine ambao wana nia nzuri na Serikali yetu,” amesema.

Alisema amemsikia Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emanuel Nchimbi akilizungumzia suala hilo na hivyo kwa kwenda pamoja kati ya chama na wabunge wanatumaini Serikali italipatia ufumbuzi jambo hilo.

“Tupo katika muda mzuri ambao tunarudi kwa wananchi, ndio mahala penyewe panapobidi tukazie ili wananchi wetu wapate amani na matumaini na ajira zao,”alisema Musukuma jambo ambalo liliwafanya wabunge kucheka.

Aprili 16, 2024 akiwa kwenye mwendelezo wa ziara mkoani Rukwa, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi aliahidi kufikisha kilio hicho kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili kitafutiwe ufumbuzi kwa kuwa ni kero kubwa kwa wastaafu.

“Tatizo la kikokotoo linalalamikiwa sana na watumishi, imekuwa kero kubwa, kuna muda lazima tuangalie wananchi wetu, wanachama wetu, tuangalie tutafika wapi, lakini kwa kadri inavyowezekana tunapaswa kutatua kero za wananchi,” alisema Dk Nchimbi.

Dk Nchimbi alisema hayo wakati akijibu swali Gilbert Kasebele aliyejitokeza kutoa kero yake mbele ya mtendaji mkuu huyo wa chama kwenye mkutano wa hadhara katika mji mdogo wa Mbalizi, mkoani Mbeya.

Akiwasilisha kero hiyo, Kasebele amesema, "mimi ni mstaafu naomba utusaidie suala la kikokotoo lilirudi kama mwanzo sio mfumo wa sasa. Mtu akistaafu basi apewe fedha zake zote, asilimia 33 inatutesa sana wastaafu.”

"Zile fedha ni za kwetu kwa nini mnatupa kidogo kidogo, nimetumikia Serikali miaka miaka 36 badala ya kunipa mafao yangu kwa mkupuo mnanipa... inaumiza na inakera naomba katibu mkuu (Dk Nchimbi), iambie Serikali ilifanyie kazi kwa niaba ya watumishi wenzangu," amesema Kasebele.


…wabunge wengine

Mbunge wa Manyoni Mashariki (CCM), Dk Pius Chaya amesema wazo la kuhamisha kikokotoo cha asilimia 50 kwa 50 na kupeleka asilimia 67 kwa asilimia 33, lilikuwa wazo jema lakini inawezekana hawakulifanyia utafiti mzuri.

“Bahati nzuri mimi nimekuwa mtumishi wa umma lakini nikastaafu mapema, nikaingia huku kwenye siasa. Inawezekana na mimi ningekuwa huko nje nami ningekuwa na hiki kilio cha kikokotoo,” amesema.

Amesema kiwango hicho cha kikokotoo, hakikuangalia matarajio ya watu na kuwa kinachosumbua kwa wafanyakazi matarajio yao waliyokuwa nayo kutotimia.

Dk Chaya amesema mfanyakazi ambaye alishaweka matarajio yake kuwa akistaafu atalipwa mafao ya mkupuo ya asilimia 50 ambayo yatakuwa Sh100 milioni lakini ghafla anaambiwa atapewa asilimia 33, hawezi kufurahia.

Amesema watumishi wengi wa umma waliopo Tamisemi ambao ni walimu na watumishi wa sekta ya afya, wamemtuma amshauri Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, aangalie upya suala la kikokotoo.

Dk Chaya amesema kama watarudisha asilimia 50 itakuwa ni tofauti ya asilimia 17 ya kiwango cha mafao ambayo anafahamu Serikali sio tatizo.

“Nikushauri tuliangalie na nimemsikia Katibu Mkuu wangu wa CCM naye ameliongelea. Ni suala ambalo linapigiwa kelele lakini tuangalie ni kitu gani tutaweka kuwapa motisha watumishi wetu,” amesema.

Ameshauri warudi na kufanya utafiti wa kutosha kuona ni njia ipi ya kusaidia wastaafu lakini kuwezesha matarajio yao.

Mbunge wa Chemba (CCM), Mohamed Monni amesema wabunge wamekuwa wanyonge sana linapoongelewa suala la kikokotoo kwa sababu ya shida wanazopata majimboni.

“Kule saa nyingine inaonekana kama jambo ambalo sisi hatuliongelei kabisa. Nikuombe sana mheshimiwa Naibu Spika tuone namna ambavyo tunaweza kufanya kama dhamira Rais ilivyo ya kurekebisha ili hali iwe salama,” amesema.

Alisema hawawezekani kuishi na watu wenye manunguniko makubwa wakati wanawasaidia kazi zao za kila siku.


Mwalimu amuuliza swali Kinana

Jana, Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Abdulurahman Kinana akiwa ziarani mkoani Mara, aliulizwa swali na Mwalimu wa Shule ya Msingi Silanga Wilaya ya Musoma Vijijini, Nyakusanya Mkangara aliyetaka chama hicho kuishauri Serikali ilegeze msimamo wake kwa kuwa kikokotoo si rafiki na kinakwenda kuwaumiza wastaafu.

Mwalimu huyo alisema kama Serikali haitaki basi kikokotoo hicho kianze kutumika kwa walimu walioanza kuajiriwa kuanzia mwaka 2018 ilipoanzishwa sheria hiyo na walimu wakongwe waendelee kutumika sheria zao za zamani.

Mwalimu Makaranga anayefundisha Shule ya Msingi Silanga A, alisema amekuwa akipata simu nyingi kutoka kwa Walimu wanaelekea kustaafu na waliokwishastaafu wakilalamikia kikokotoo.

Akijibu hoja hiyo, Kinana alisema kutokana na malalamiko ya kikokotoo kutokea nchi nzima, chama hicho kitakuja na majibu sahihi baada ya kukaa kwenye vikao vyao vya ndani.

"Malalamiko yapo na yanaendelea kuongezeka, lazima tuwe na majibu sahihi ya jambo hilo na mimi nalichukua ndugu mwenyekiti wa walimu naenda kushirikiana na wenzangu kulijadili vizuri kuona njia nzuri inayofaha," amesema.

"Sijuhi kama mlisikia, mimi nimesikia sana habari ya kikokotoo kinapigiwa kelele nchi nzima, jambo moja ambalo limetamkwa hadharani na Katibu Mkuu wa Chama Dk Emmanuel Nchimbi atalifikisha kwa Mwenyekiti wa Chama na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan," amesema.

"Kwa maana nyingine jambo hili atalifikisha kwenye vikao vikuu vya chama litajadiliwa kwa sababu linapigiwa kelele na hatuwezi kujidai hatujui na wala hatujasikia na hatuwezi kujidai hatuna habari," amesema