Wabunge walia na madeni ya makandarasi, bili za maji

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2025 / 2026 jijini Dodoma leo Mei 8, 2025
Muktasari:
- Wataka madeni ya bili za maji na wakandarasi yawe yameshalipwa hadi kufikia mwishoni mwa Juni 2025.
Dodoma. Kilio cha taasisi za umma kulimbikiza madeni ya huduma za maji na madai ya makandarasi kimezua mjadala bungeni wakati wa kujadili makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Awali, akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Jackson Kiswaga, ameeleza changamoto sugu ya baadhi ya taasisi za umma kushindwa kulipa ankara za maji kwa wakati, hali inayozorotesha uwezo wa mamlaka za maji kujiendesha.
Kiswaga amezitaja taasisi tisa zinazodaiwa jumla ya Sh61.42 bilioni na mamlaka za maji kuwa ni Jeshi la Magereza (Sh11.08 bilioni), JWTZ (Sh34.51 bilioni), Jeshi la Polisi (Sh10.98 bilioni), hospitali za mikoa chini ya Wizara ya Afya (Sh1.68 bilioni), Mifugo na Kilimo (Sh225.05 milioni), Ikulu Ndogo (Sh287.81 milioni), Serikali za Mitaa (Sh2.44 bilioni), Maliasili na Utalii (Sh122.30 milioni), na Mahakama (Sh61.40 milioni). Kamati imetaka madeni hayo yalipwe kabla ya Juni 30, 2025.
Aidha, kamati imesisitiza umuhimu wa Serikali kulipa deni la makandarasi linalofikia Sh534.72 bilioni kabla ya tarehe hiyo.
Kiswaga ameonya kuwa kuchelewesha malipo kunachelewesha au kukwamisha miradi ya maji, kuongeza gharama kwa Serikali, na kupunguza imani ya wananchi kwa Serikali yao, sambamba na kuathiri wakandarasi wadogo wa ndani.
Akichangia hoja, Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya, amelalamikia hali hiyo, akisema haingii akilini kuona taasisi zinadaiwa Sh61 bilioni huku wananchi wakikatiwa maji kwa kuchelewa kulipa bili ndogo.
Hivyo, amemtaka Waziri Aweso kuchukua hatua kali, zikiwemo kuzikatia maji taasisi hizo.
Aidha, ameshauri Wizara ya Fedha kuelekeza fedha kwenye Mfuko wa Maji ili kulipa makandarasi na kuwezesha miradi ya maendeleo inayolenga kuondoa adha kwa wanawake wa vijijini.
Mbunge wa Kinondoni, Abbas Tarimba, amesema mradi wa maji wa bwawa la Kidunda umefikia asilimia 28 na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) ilisema ujenzi ulikuwa ukamilike Juni 2026.
Amesema kutokana na fedha kupatikana kidogo kidogo na kwa kuwa mradi huo unatumia fedha za ndani, inawezekana mradi huo ukaenda hadi mwaka 2027, jambo ambalo pia linategemea upatikanaji wa fedha.
Amesema alipata faraja kwa kuwa wameanzisha mazungumzo na Benki ya TIB, ambayo imesema iko tayari kutoa fedha kwa ajili ya mradi huo, na kuwa Tume ya Taifa ya Mipango imeshakubaliana nao.
Tarimba amesema kuwa hoja hiyo sasa ipo Wizara ya Fedha ikisubiri maamuzi, na kumtaka Waziri Aweso kuwa king’ang’anizi ili apate fedha hizo, kwa sababu hadi sasa makandarasi wanadai kwenye mradi huo.
“Mpaka leo hivi ninavyozungumza, makandarasi wanaotekeleza mradi wa maji wa Kidunda wanadai Sh32.2 bilioni, na washauri wanadai Sh1.56 bilioni,” amesema.