Wadaiwa kuiba mamilioni kwenye gari Moshi
Muktasari:
- Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linafuatilia tukio la wizi wa mamilioni ya fedha ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa nje ya moja ya maduka makubwa yaliyopo katikati ya mji wa Moshi na kutokomea na fedha hizo kusikojulikana.
Moshi. Watu wanaodhaniwa kuwa wezi wamevamia na kuiba mamilioni ya fedha yanayodaiwa ni mali ya kampuni ya Charan singh & Sons ltd katika tukio lililonaswa na kamera za usalama (CCTV Camera), eneo la tukio katikati mji wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.
Fedha hizo ambazo kiasi chake hakijawekwa wazi, zimeibiwa ndani ya gari inayodaiwa ni mali ya kampuni hiyo wakati lilipoegeshwa katika moja ya maduka makubwa (supermarket) yaliyopo katikati ya mji wa Moshi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana kutoka eneo hilo, jana Jumatano asubuhi, Novemba 22,2023, wakati walipoliegesha gari nje ya duka hilo lililopo mtaa wa Boma road na kuingia ndani, ndipo watu hao walipoingia na gari lao na kisha kuegesha pembezoni mwa gari hilo na kuiba fedha hizo.
Hata hivyo, leo Alhamisi Novemba 23, 2023 katika mitandao ya kijamii ilionekana video iliyonaswa na moja ya CCTV Camera iliyopo eneo hilo ikionyesha namna watu hao walivyoingia eneo hilo na kubananisha gari lao na gari lililokuwa na fedha hizo na muda mfupi baada ya kutekeleza tukio hilo na kuondoka na gari lao kusikojulikana.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa kwa simu amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza hawezi kulizungumzia kwa undani kwa kuwa uchunguzi unaendelea.
"Ni kweli waliibiwa fedha kwenye gari, bado tunafuatilia na ikikamilika tutaitolea taarifa," amesema.
Akizungumzia tukio hilo, ofisa rasilimali watu wa kampuni hiyo, Jefta Siao mbali na kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo, hakuwa tayari kueleza kiasi cha fedha kilichoibiwa akieleza tayari wamekabidhi suala hilo kwa vyombo husika ikiwemo polisi ambao wanaendelea na uchunguzi.
"Huenda wezi wale walimuona mhusika akitokea benki, kwani mtu akiingia benki kuna watu wanaokuwa wamekaa pembeni kuangalia kinachoendelea na anakuvizia, picha za kamera zinavyoonekana, ni kwamba walimuona akitokea benki na hizi ni nyakati za Krismasi watu wanatafuta fedha kwa namna yoyote ile," amesema.
Aidha, alipoulizwa kwa nini hawakuwa na ulinzi kutokana na kiasi hicho walichokwenda kuchukua benki, amesema tukio hilo limewapa funzo na wataendelea kufuata ushauri ili kuhakikisha tukio kama hilo halijirudii.