Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau wa kodi watofautiana mkataba kati ya Tanzania, UAE makubaliano ya kodi

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba na Waziri wa Nchi wa Mambo ya Fedha wa Nchi za Falme za Kiarabu, Mohamed Bin Hadi Al Hussaini wakionyesha mkataba wa makubaliano ya kuondoa utozaji kodi mara mbili na kuzuia ukwepaji wa kodi ya mapato kati ya nchi hizo mbili, baada ya kutiliana saini mjini Dubai, Falme za nchi za Kiarabu. Picha na WFM

Muktasari:

  • Baada ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kusaini makubaliano ya kuondoa utozaji kodi mara mbili, wadau wametoa maoni tofauti kuhusu faida na hasara za mikataba ya aina hiyo.

Dar es Salaam. Baada ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kusaini makubaliano ya kuondoa utozaji kodi mara mbili, wadau wametoa maoni tofauti kuhusu faida na hasara za mikataba ya aina hiyo.

 Jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisaini mkataba huo na wa kuzuia ukwepaji wa kodi ya mapato akiiwakilisha Tanzania pamoja na Waziri wa Fedha wa UAE, Mohamed Bin Had Al Hussain.

Makubaliano hayo yanalenga kuhamasisha uwekezaji utakaochochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha kipato cha wananchi wa pande hizo mbili.

Waziri Nchemba alisema kusainiwa kwa mkataba huo ni jitihada za kuondoa changamoto za biashara ili kukuza mahusiano ya kiuchumi, kuimarisha ushirikiano wa kodi na kuchochea mazingira wezeshi ya uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

“Ni matumaini yetu kwamba baada ya mkataba huu tutaona uwekezaji mkubwa ukikua kati ya nchi zetu hizi, hasa kutoka Uarabuni ambao wana mitaji mikubwa, lakini utozaji kodi mara mbili ulikuwa unawakwaza,” alisema Dk Nchemba.

Mkataba huo wa makubaliano ya kodi ni wa 10 kwa Tanzania. Mingine ni kati ya Tanzania na Afrika Kusini uliosainiwa mwaka 2005, Canada 1995, nchi za Scandinavia zinazojumuisha Denmark, Finland, Norway, Sweden zote mwaka 1976, India 1979, Italia 1973 na Zambia 1969. UAE yenyewe imeingia mkataba kama huo na nchi 139.


Wadau wa kodi watofautiana

Mtaalamu wa uchumi na kodi, Dk Balozi Morwa alitahadharisha kuwa huenda mikataba hii ikawa chanzo cha nchi kupoteza mapato kutokana na makubalino yake kuwa ya ‘Nitoze ushuru ninapofanya biashara Tanzania, lakini sio ninapofanya biashara na Tanzania’.

Alisema; “Hakuna tofauti yoyote iliyoonyesha kama tumewahi kunufaika na mikataba hii licha ya kuwa tunayo muda mrefu”.

Dk Morwa, ni mhadhiri mwandamizi Chuo Kikuu cha Katoliki Mbeya (CUCoM) alieleza kuwa tafiti zinaonyesha hakuna mwekezaji anayewekeza kwa sababu za kodi.

“Watu hawana tatizo na kulipa kodi, jambo kubwa kwa wawekezaji ni usalama wa mitaji yao na miundombinu ya uwekezaji, sababu ya kodi inakuja baadaye sana,” alisema na kuhadharisha mikataba hii ni hatari zaidi kwa vitu vinavyoisha kama madini na vivutio vya utalii.

Kwa upande wake, mtaalamu wa masuala ya kodi, Martin Chambai alisema nchi inaweza kuingia mkataba wa namna hii sio kwa faida za kikodi pekee. “Zipo faida nyingine za kiuchumi, mwekezaji anaweza kujenga kiwanda akazalisha ajira na kuwawekea uhakika wafanyabiashara wengine wa malighafi kwa nchi husika.

“Mfano ni Serikali ya nchi ya Ireland, Jumuiya ya Ulaya (UE) na kampuni ya Apple. EU waliitaka Ireland kuitoza kampuni hiyo kodi, lakini kutokana na faida za kiuchumi zilizotokana na kampuni hiyo hawakufanya hivyo,” alisema.


Zaidi kuhusu mkataba huo

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru alisema: “Baadhi ya watu wanaweza kutafsiri kuwa mikataba ya aina hii ni kusamehe kodi, la hasha, hii ni mikataba inayoweka kanuni ya kuzuia uhamishaji wa kodi kutoka nchi moja kwenda nyingine kwa kuzingatia uwekezaji unatoka katika eneo gani, inahusisha kulinda mitaji ya wawekezaji wa nchi husika,” alisema Mafuru.

Kwa mujibu wa mtandao wa Tranding Economics, biashara baina ya Tanzania na UAE ilikadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani 871 milioni (wastani wa Sh2.001 trilioni).

Baadhi ya bidhaa zinazohusika zaidi ni vito, madini, mbogamboga, dawa za asili, samaki, kahawa, chai, viungo, matunda, manukato na vipodozi.