Wadau wachambua kufeli wanafunzi kidato cha pili, darasa la nne

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Wadau washauri kufanyike maboresho kuinua kiwango cha elimu kwa wanafunzi wa kidato cha pili na darasa la nne, ili kupunguza wimbi la wanaofeli mtihani wa Taifa.

Dar es Salaam. Wadau wa elimu nchini wamependekeza kufanyike maboresho  kuinua kiwango cha elimu kwa wanafunzi wa kidato cha pili na darasa la nne ikiwamo kuondoa msongamano darasani.

Pia, wamependekeza kudhibiti nidhamu ya mwanafunzi, kuboresha mitalaa, kuandaa vifaa vinavyohitajika kwa mwanafunzi kujifunza na kuandaliwa walimu wenye uwezo wa  kufundisha.

Mapendekezo hayo wameyatoa usiku wa leo Jumatano, Januari 10, 2024 kwenye mjadala wa Mwananchi X (zamani Twitter), uliokuwa na mada ya ’Nini kifanyike kupunguza wanafunzi kufeli darasa la nne, kidato cha pili?’

Msingi wa mada hiyo ni matokeo ya kidato cha pili na darasa la nne yaliyotangazwa Jumapili ya Januari 7, 2024 na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta).

Katika matokeo ya darasa la nne, wanafunzi 1,287,934 sawa na asilimia 83.34 wamefaulu kuendelea na darasa la tano.

Upande wa kidato cha pili, wanafunzi 592,741 ambao ni sawa na asilimia 85.31 wamefaulu kwa daraja la kwanza hadi la nne.

Katika mjadala wa X, wadau hao wameeleza mapendekezo hayo yakizingatiwa yasaidia kupunguza wimbi la wanafunzi kufeli mtihani wa Taifa.

Akichokoza mada hiyo, Mwandishi wa Habari za Elimu Gazeti la The Citizen, Jacob Mosenda amesema kupunguza msongomano darasani kunaweza kusaidia, kwa kuwa baadhi ya shule za Serikali zina wanafunzi wengi ikilinganishwa na idadi ya walimu wanaotakiwa kuwafundisha.

“Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili mwaka jana pamoja na changamoto zingine katika ripoti hiyo iliyoangazia matokea ya kidato cha pili inaonyesha kuna shule zina wanafunzi wengi na walimu kidogo na wanachokifanya walimu ni kutekeleza wajibu wao tu,” amesema.

Mosenda amesema hata suala la nidhamu linapaswa kudhibitiwa kuanzia kwa wazazi kwa kuangalia mazingira wanayoishi huku akieleza katika uchunguzi huo, ulibaini kuna wanafunzi wanavuta bangi na kusababisha nidhamu kuendelea kushuka.

“Mambo yote hayo yanatakiwa kuanzia kwa wazazi kwa kuangalia namna wanavyoishi na watoto kama anaishi naye nyumba moja halafu anafanya mambo yasiyokuwa na maadili wanaharibu hadi ndoto za watoto,” amesema.

Mwandishi na Mtumzi wa Vitabu, Richard Mabala amekiri kuna ukosefu wa maadili huku akigusia matokeo 26 kati ya 32 ya shule za Serikali wanafunzi karibu laki moja walipata alama D au kufeli.

“Tunapopeleka lawama kwa wazazi na wanafunzi kwangu ni kosa, tuangalie na  mitalaa ni kweli unaendana na umri wa wanafunzi, kuna kitu kwenye elimu yetu inaangalia kukariri tu,”amesema.

Katika maelezo yake amesema kuna tafiti ziliandikwa, kiwango cha lugha kinachotumika hakiendani na lugha wanayoelewa wanafunzi kwa urahisi.

“Sasa mtihani unalenga kiwango cha uelewa wa mwanafunzi. Je? walimu wameandaliwa kuangalia masomo hayo kwa mujibu wa mitalaa hiyo, vyote hivyo inabidi viangaliwe,” amesema.

“Mimi naona kuna uhaba wa vitabu, madarasa na walimu waliandaliwa kufundisha masomo hayo, nikirudi kwenye mitihani je ina umuhimu gani wanasema unapima maendeleo ya mtoto kweli wanapima maendeleo au uwezo wa kukariri.

“Kidato cha pili, mtoto anatoka darasa la saba hana Kiingereza haya basi unasema afundishwe wiki sita Kiingereza hiyo inatosha, kwanini tunaendelea kufundisha watoto kwa lugha wasiyoelewa,” amesema

Katika mjadala huo, Dk Mark Mringo ametaja mambo mengine matatu ya kuangalia, kwanza ni kiasi gani jamii ina kiu na inajivunia elimu kama mkombozi wa fikra.

“Mfano sasa hivi kuna uchizi wa mpira, Tanzania ikiifunga Misri nchi inasisimka je, kwenye elimu tupo hivyo? Kwa hiyo kuna namna hakujawekwa kipaumbele kwenye elimu,” amesema.

Dk Mringo ametaja jambo lingine walimu wa kufundisha watoto, baadhi yao hawana uwezo wa kutumia mbinu zaidi za kuwafanya waelewe maarifa yanayotolewa, badala yake wameamua kufanya bora liende hawajitumi.

“Vijana wetu wanaoingia sekondari na vyuo vichwa vimejaa vitu vingine kazi inayofanyika ni kuondoa vitu vilivyopo kichwani, kuingiza vitu vipya, elimu sasa sio 1+1 ni mbili, bali ni malezi,” amesema na kuongeza

“Mzazi, mwalimu vifaa na mwanafunzi vyote vikienea elimu inatokea, vikipelea wapo watakaojielimisha lakini si lazima kuwa navyo utakavyowapima, namaanisha hivi kwa mfano mtoto asiyejua kusoma na kuandika ukimpa simu anaweza kufanya jambo kubwa zaidi,” amesema.

Naye mshauri wa masuala ya elimu wa Shirika la Hakielimu, Dk Wilberforce Meena amesema lengo linalozungumzwa mtihani wa darasa la nne na kidato cha pili ni kuelewa umahiri wa wanafunzi na walimu wawasaidie wanafunzi kwa darasa linalofuata.

“Nilitegemea ndio malengo ya upimaji huo. Huwa najiuliza mwanafunzi aliyepata daraja la kwanza kidato cha pili anaweza kupata daraja sifuri kidato cha nne,” amehoji katika mjadala huo.

Amesema upimaji huwa kila siku haufanani na walimu waliopo nchini na aina ya mazoezi wanayofundishwa wanafunzi unatofautiana.

“Nilikuwa nawaza kidato cha pili wangefanyiwa upimaji kulingana na masomo waliyosoma na si kuwalinganisha na wanafunzi wa shule zingine, nilitegemea matokeo haya yaliyotangazwa yangetueleza hao wanafunzi wana changamoto katika maeneo gani,” amesema.

Katika maelezo yake, amesema kubainisha maeneo hayo itawasaidia walimu kujua wana shida gani ili wawasaidie.

 “Sasa hii ina shida kwa sababu upimaji wake unafanywa kama mtihani wa Taifa na haumsaidii mwalimu kujua shida ya mwanafunzi,” amesema.

Amebainisha hatupaswi kuwalaumu wanafunzi kwa sababu asubuhi wanakwenda shuleni kwa furaha na wanawakuta walimu, isipokuwa jamii inapaswa kujiuliza wanaopimwa, wamefikia hatua ya kupimwa.

“Ufanisi wetu wa elimu sio mzuri huwezi kuwa na wanafunzi zaidi ya laki moja ambao hawakufanya mtihani, kwa hiyo ninachosema ufanisi katika elimu upo chini na upimaji wetu unakosa uhalali kwa wanafunzi wetu,” amesema.

Naye Mdau wa elimu, John Sebastian amesema suala la watoto kufanya vibaya kwenye mtihani ni jambo linalopaswa kuangaliwa kwenye mnyororo, kuanzia mtoto anavyokwenda shule na namna anavyosoma kujiandaa kujibu mtihani.

“Mazingira kutoka nyumbani hadi kufika shuleni ni umbali gani, shuleni anakutana na watu wa namna gani, mazingira ni rafiki na je, ana utulivu?

“Sasa nini kifanyike ni muhimu tuwe na kiasi kidogo lakini ni bora, Serikali inagharamie elimu kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita na ikifanya hivyo isiache wananchi wachangie kuanzia kidato cha nne mpaka sita,” amesema.

Jambo lingine ameshauri walimu warudi kwenye majukumu yao, hawawezi kumuona mwanafunzi amenyong’onyea halafu ukaendelea kutulia, “ukimuona mtoto yupo tofauti lazima umsaidie kwa wakati…sasa swali mwalimu ana motisha ya kufanya hivyo.”