Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu za kufeli wanafunzi ni zile zile - (1)

Muktasari:

Ulalamikaji huu huhusu sehemu kubwa ya wazazi ambao watoto wao husoma shule za Serikali na baadhi ya shule za binafsi ambazo hazijajipanga vya kutosha.

Tangu tupate Uhuru mwaka 1961 tumekuwa na kawaida ya kushangaa na kushtuka kila matokeo ya wanafunzi wa shule zetu yanapotolewa na mamlaka inayotunga na kusimamia mitihani ya Taifa, yaani Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).

Ulalamikaji huu huhusu sehemu kubwa ya wazazi ambao watoto wao husoma shule za Serikali na baadhi ya shule za binafsi ambazo hazijajipanga vya kutosha.

Niliona nitumie darubini hii kuzungumzia sababu zinazofanya wanafunzi wa ngazi mbalimbali wapate matokeo mabaya kwenye mitihani yao. Kwa hakika, sababu ni zilezile na kwa hiyo nitaeleza yaleyale ambayo sote tunayafahamu, lakini tumekuwa tunayapuuza.

Katika mfululizo wa makala haya nitaongelea sababu zifuatazo ambazo ni makosa yanayosababisha watoto kushindwa mitihani; kwanza ni makosa ya jumla yanayofanywa na Serikali, pili ni makosa ya Serikali kwa walimu, tatu ni makosa ya Serikali juu ya elimu, nne ni makosa ya wazazi na jamii na mwisho nitazungumzia sababu zinazofanya shule binafsi zifaulishe watoto kwa uhakika zaidi.

Katika makala ya leo tutaanza na sababu au makosa ya jumla ambayo Serikali imekuwa ikiyafanya na baadaye yanakuwa kizingiti cha elimu na hivyo kuleta athari katika taaluma na kuwafelisha watoto.

 

Ukosefu wa mazingira rafiki

Kati ya mambo ambayo Serikali yetu haijafanya kwa uhakika ni ujenzi wa shule bora kwa ajili ya watoto. Tumejenga shule nyingi kila mahali nchini, lakini ukipima ubora wa shule hizo unagundua kuwa zinachangia kutowapa fursa ya kutosha watoto kushiriki katika mambo yote muhimu yanayohitajika kumfanya mtoto asome kwa utulivu na baadaye kufaulu.

Shule yenye mazingira rafiki kwa mtoto ni ile ambayo imejengwa kitaalamu na kila ukionacho hapo shuleni kimepangwa kiustadi; madarasa ya kutosha, mapana, yenye hewa na yanayosafishika kirahisi, viwanja vya michezo ya kila aina ili kumfanya kila mtoto awapo shuleni aweze kushiriki mchezo autakao au aupendao.

Kwa bahati mbaya shule nyingi za Serikali zina viwanja viwili tu, kiwanja cha mpira wa mikono na cha mpira wa miguu. Wapo watoto kwa mamia ambao hupenda pia kushiriki kwenye michezo majira ya jioni au mwishoni mwa wiki na hivyo kutumia muda wa ziada baada au kabla ya michezo kujisomea hapo shuleni.

Kukosekana kwa viwanja vya michezo mbalimbali kunawafanya baadhi ya watoto washindwe kuvutiwa na kukaa shuleni muda mrefu na hivyo huishia mitaani kila wanapomaliza vipindi na huko hawasomi tena kwa utulivu.

Shule bora huwa na maabara za uhakika, siyo moja tu, maabara kadhaa kutokana na michepuo iliyoko shuleni hapo. Nilipokuwa shule ya sekondari tulikuwa na maabara moja na nakumbuka walimu waligongana na kuigombania, walimu wa kidato cha kwanza wawapeleke watoto wote humo humo, wa kidato cha pili, cha tatu na cha nne waliitaka pia, haiwezekani!

Shule bora na nzuri huwa na maabara kwa ajili ya somo la Biolojia, maabara kwa ajili ya somo la Fizikia na hata nyingine kwa ajili ya Kemia, hii inafanywa ili pindi walimu wengi wa masomo yanayotumia maabara wanapohitaji kutumia maabara iwe rahisi kuwagawa na kuwafanya waenende na kasi inayohitajika kukamilisha mitaala.

Uwapo wa maabara unapaswa kwenda sambamba na wataalamu wa maabara hizo, watunzaji wa vifaa na watu ambao hata kama mwalimu wa somo hayupo wanaweza kuwasaidia wanafunzi wa michepuo mbalimbali muda wote kufanya mafunzo katika maabara husika.

Kama hatuwekezi huko tutashindwa kuzalisha wanasayansi wa uhakika na wa kutosha, bali watoto wetu wataendelea kufanya vibaya, hasa katika masomo ya sayansi.

Je, shule ambayo anasoma mtoto wako ina maktaba. Hakika, hadi mwaka 2012 ni shule tatu tu kati ya 10 za Serikali zilikuwa na maktaba, hivi sasa inawezekana kuwa shule tano kati ya 10 zikawa na maktaba, lakini hizo zenye maktaba lazima zitakuwa zinakabiliwa na upungufu mkubwa wa vitabu vya kiada na ziada na kwa hiyo watoto hawawezi kuchota maarifa.

Zipo wilaya ambazo si tu hazina maktaba kwenye moja ya shule zake, lakini hazina hata maktaba ya wilaya na kwa hiyo watoto wa wilaya hizo hawajui watafanyaje kuchukua maarifa ya ziada nyakati ambazo wako shuleni ama likizo, hii ni sababu zinazofelisha watoto wetu kwa nguvu.

Hali ya utoaji wa chakula kwenye shule zetu, pamoja na maji ya kunywa inasikitisha. Shule nyingi za Serikali hazitoi chakula cha mchana na hazina maji safi ya kunywa.

Watoto wengi wanaathirika kisaikolojia linapokuja suala la kukosa huduma muhimu ambazo wangelitamani wazipate. Shule zinazotoa chakula shuleni zinakuwa chachu ya watoto kubakia shuleni na kuendelea kujisomea kwenye vikundi na binafsi, shule zisizotoa chakula cha mchana ni sawa na mzazi anayemfukuza mtoto wake nyumbani akalale porini.

Shule hizi huwafanya watoto waondoke shuleni kwa lazima ili wakajipikie au kuwahi chakula cha nyumbani, hali hiyo huwatoa kwenye ari ya kujisomea na matokeo yake yanajulikana. Nimegusia maji ya kunywa kwa sababu mtoto mwenye kiu hawezi kujishughulisha na kuwekeza akili masomoni, atawaza wapi anapata maji safi, hayapo! Ni sawa na mwanafunzi mwenye njaa, anawezaje kufundishika? Mwanafunzi mwenye kiu shuleni na yule mwenye njaa hawawezi kufanya lolote la maana.

Ni sawa na mtu mzima mwenye familia, nyakati ambazo hauna senti tano mfukoni, kila kitu hakiendi na hata akili inasimama. Kuwanyima watoto wetu maji ya kunywa na chakula cha mchana kwenye shule zetu ni kuzifanya akili zao zisimame na kutochota maarifa mapya mwaka mzima.

 

Ukosefu wa vifaa na walimu

Utafiti wa taasisi ya Twaweza wa mwaka 2012 unaonyesha kuwa kuna tofauti kubwa kimkoa kati ya idadi ya wanafunzi wanaotumia kitabu kimoja cha kiada.

Dar es Salaam kwa mfano, wanafunzi 14 wanatumia kitabu kimoja ikilinganishwa na wanafunzi 41 kwa kila kitabu mkoani Kigoma. Hata mkoa wenye kufanya vizuri kama Dar es Salaam, bado wanafunzi wengi hutumia vitabu vichache, yaani kitabu kimoja watoto 14.

Hiyo inatufundisha nini? Safari ni ndefu, tunagutuka watoto wakifeli lakini tunasahau kuwa kuna majukumu hatukuyatimiza. Watoto 41 watumie kitabu kimoja kwenye shule ya Serikali, kisha watoto hao wakashindane katika mtihani mmoja na washindani wao ni watoto wanaotoka shule zinazotumia kitabu kimoja mtoto mmoja, haiwezekani na kwa hiyo suala la ukosefu wa vitabu vya kiada kwenye shule za Serikali linachangia kwa kiasi kikubwa kufelisha wanafunzi na hiyo inamaanisha kama halichukuliwi hatua tusitegemee maajabu.

 

Uchache wa walimu

Hakika, walimu walioko kwenye shule za Serikali ni wachache kupita kiasi. Siku moja nimewahi kuona kwenye televisheni, shule moja mkoani Mtwara ina wanafunzi zaidi ya 200 wa sekonndari na ina walimu wawili, mwalimu wa Kiingereza na Historia ambaye pia amejikasimu kufundisha Uraia, Kiswahili na Jiografia kidato cha kwanza hadi cha tatu.

Mwalimu wa pili ambaye ni mwalimu mkuu akifundisha Fizikia na Kemia, lakini akijikasimu kufundisha Hisabati na Biolojia. Walimu wawili wanafundisha masomo yote kidato cha kwanza hadi cha tatu na wao ndiyo walimu wa zamu, wao ndiyo Mwalimu Mkuu na Mwalimu Mkuu msaidizi na wafanyakazi wa shule. Haiwezekani.

Julius Mtatiro ni mchambuzi wa masuala ya kijamii na kisiasa, mtafiti na mwanasheria. Simu; +255787536759/ Baruapepe; [email protected]/ Tovuti; juliusmtatiro.com