Wadau waja na mapendekezo ripoti ya Kichere

Wadau waja na mapendekezo ripoti ya Kichere

Muktasari:

  • Baadhi ya wasomi na wadau wameishauri Serikali kuyafanyia kazi mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere aliyoyatoa kwenye ripoti ya ofisi yake kwa Bunge.

Dar es Salaam. Baadhi ya wasomi na wadau wameishauri Serikali kuyafanyia kazi mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere aliyoyatoa kwenye ripoti ya ofisi yake kwa Bunge.

Juzi, CAG aliweka hadharani ripoti hiyo ya ukaguzi iliyoainisha matumizi mabaya ya fedha za Serikali, huku akibainisha kasoro kwenye miradi mingi inayoendelea kutekelezwa na iliyokamilika lakini haitumiki.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, wasomi na wadau hao wa uchumi nchini walisema endapo Serikali itakuwa na nia ya kupambana na rushwa, inabidi iyatumie vyema mapendekezo ya CAG anayotoa katika sekta mbalimbali.

“Wayafanyie kazi ili kubaini mianya ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka na rasilimali za umma na mikataba mibovu isiyo na tija kwa taifa,” alisema Faraja Kristomus, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Alisema ili mapendekezo hayo yasaidie nchi, ni budi kuandaliwe bango kitita kitakachokuwa na vipengele vitano vya kueleza tatizo lililoibuliwa, mhusika aliyetenda kosa, hatua ya kuchukuliwa na mhusika sambamba na muda wa kutekelezwa bila kusubiri ripoti nyingine.

Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema miaka iliyopita walikuwa wakihoji ununuzi wa ndege ambazo Serikali ya awamu ya tano iliyafanya lakini majibu hayakuwa wazi.

Alisema ni kawaida kwa Shirika la Ndege kupata hasara na mashirika mengi duniani yamepata hasara.

“CAG ameeleza katika ripoti yake kwamba bodi ya wakurugenzi ya ATCL haina hata mjumbe mmoja mwenye ujuzi wa mambo ya anga, sasa hapo tutegemee nini?” alihoji Zitto.

Wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke alisema kitendo cha CAG kuweka hadharani kasoro alizozibaini kwenye taasisi na miradi mikubwa ya maendeleo, kinaonyesha namna ya uwazi ambao kuna urahisi wa kupambana na rushwa.