Wadau, wanahabari wamlilia Ubwani akiagwa, kuzikwa kesho kijijini kwao Katesh

Mwakilishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Daniel Mjema,akitoa heshima za mwishokwenye mwili wa  aliyekuwa mwandishi wa habari wa gazeti la The Citizen mkoani Arusha, Zephania Ubwani ambaye ameagwa nyumbani kwake leo Jumanne Aprili 9,2024 eneo la ,Kimandolu jijini Arusha.

Muktasari:

  • Ubwani ambaye alifanya kazi kwa muongo mmoja na kampuni ya Mwananchi Communications  Limited (MCL) alifariki dunia Aprili 6,2024  wakati akiwa kwenye majukumu yake ya kazi katika hoteli ya Kibo Palace, Mkoani Arusha.

Arusha. Wadau wa Kitaifa na Kimataifa wamemlilia na kuelezea alama alizoziacha katika tasnia ya habari aliyekuwa Mwandishi wa habari Mwandamizi wa Gazeti la The Citizen mkoani Arusha, Zephania Ubwani (70) aliyefariki dunia Aprili 6, mwaka huu

Wamesema licha ya umri mkubwa aliokuwa nao, alikuwa ni mtu wa kujituma na kufanya kazi kwa umakini na mwalimu kwa wengine.

Ubwani ambaye amefanya kazi kwa muongo mmoja na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), alifariki dunia Aprili 6,2024 wakati akitekeleza kazi yake ya uandishi wa habari katika Hoteli ya Kibo Palace, jijini Arusha.

Akitoa salamu za rambirambi, Ofisa Uhifadhi Mwandamizi kitengo cha Mawasiliano cha Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Catherine Mbena amesema Ubwani alikuwa mwandishi aliyejituma katika kazi yake na alikuwa balozi mzuri wa mazingira na uhifadhi.

Amesema licha ya kujituma lakini ameacha alama isiyofutika katika tasnia ya habari kutokana na umahiri aliokuwa nao na uchapakazi wake.

"Zephania (Ubwani) alikuwa mwandishi mahairi sana, mimi wakati nakuja kwenye kituo changu cha kazi hapa Arusha alikuwa miongoni mwa waandishi niliowakuta, alikuwa akijituma katika kazi, hakuwa mwandishi tu wa Arusha bali wa Tanzania, hakika tutamkumbuka kwa mengi mzee wetu, ameifanyia mambo makubwa tasnia ya habari," amesema Mbena.

Mwakilishi kutoka Mahakamani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACJ), Anna Nabaasa amesema kama Jumuiya watamkumbuka kwa kazi nzuri alizofanya enzi za uhai wake katika Jumuiya hiyo kupitia Taasisi zake ikiwemo Bunge la Afrika Mashariki na Mahakama hiyo.

"Sisi kama Jumuiya tumempoteza mwandishi ambaye aliandika vizuri katika Jumuiya yetu na tulipopata taarifa za msiba wake tuliumia sana na kujiuliza tutapata wapi mwandishi mzuri kama Zephania (Ubwani) ambaye ataweza kuiandikia EAC, hilo ni pigo kubwa kwetu lakini na jamii kwa ujumla,” amesema Nabaasa.

Amesema habari nyingi alizoandika zilitengeneza vichwa vya habari vizuri vilivyovuta wasomaji wengi.

Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania ( TCCIA), Mkoa wa Arusha, Walter Maeda amesema;

"Tunamshukuru Mungu kwa kutupa mtu kama Zephania, tulikuwa hatumtumii habari, bali alikuja kutafuta habari mwenyewe. Nakumbuka kipindi malori yamekwama mpakani Namanga, alikuja kutuambia kuna tatizo tafuteni suluhu kwa sababu sisi tuko EAC ila naona Muungano unataka kuvurugwa, tukachukua hatua,” amesimulia Maeda.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari jijini Arusha, Mussa Juma akitoa salamu zake amesema watamkumbuka Ubwani kwa kuwa alikuwa kiunganishi kwa waandishi wa habari na alikuwa akitoa ushauri pale wanapokwama kwenye masuala yanayohusu habari.

"Tutamkumbuka sana Ubwani kwa kuwa alikuwa mtu mwenye upendo mkubwa na waandishi wa habari hata tunapokwama kwenye masuala yetu ya habari, alikuwa kinara wa kutuelekeza na hata tulipokwaruzana yeye ndiye aliyesimama na kutusuluhisha, hakika tumepoteza kiungo muhimu katika tasnia yetu, tangulia Mzee Ubwani, kazi ya Mungu haina makosa,” amesema Juma.

Ubwani aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 70, ameacha mjane na watoto wanne.