Wadau wapanda miti 500 kupambana na ukame Moshi
Mratibu wa Masoko na Mauzo kutoka kampuni ya Bonite bottlers, Leornard Makule akikabidhi mche wa mti kwa mkuu wa shule ya Sekondari ufundi ya Moshi TEC, mwalimu Philipo Mwanga.
Moshi. Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha uoto wa asili, wadau wa mazingira mkoani Kilimanjaro wamekabidhi miche zaidi ya 500 kwa Shule ya Sekondari ya Ufundi Moshi TEC, iliyopo Wilaya ya Moshi.
Miche hiyo, ikijumuisha miti 200 ya matunda na 300 ya kivuli, imepandwa kuzunguka maeneo ya shule hiyo kwa lengo la kuboresha mazingira na kuchangia lishe bora kwa wanafunzi.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano, Mratibu wa Masoko na Mauzo kutoka Kampuni ya Bonite Bottlers, Leornard Makule, alisema hatua hiyo ni sehemu ya juhudi endelevu za kampuni hiyo katika kutunza mazingira ya Mkoa wa Kilimanjaro, hususan maeneo ya mlima Kilimanjaro.
“Tulipokea ombi kutoka kwa shule na kwa kuwa sisi ni wadau wa mazingira, tumeona ni vyema kutoa miche hii ili kusaidia kurejesha uoto wa asili, lakini pia kuboresha lishe ya wanafunzi kupitia matunda,” amesema Makule.
Amesema tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo mwaka 1987, Bonite Bottlers imekuwa mstari wa mbele kushirikiana na taasisi mbalimbali kuhifadhi mazingira ya mkoa huo.
“Tumejikita katika kulinda na kuendeleza mazingira ya Mlima Kilimanjaro kwa kushirikiana na taasisi za serikali na mashirika binafsi,” ameongeza Makule.
Kwa upande wake, Mkuu wa shule hiyo, Philipo Mwanga, alisema kupandwa kwa miti hiyo kutasaidia kubadili sura ya mazingira ya shule hiyo ambayo hapo awali yalichakaa kufuatia miti mingi kukatwa wakati wa ujenzi wa miundombinu.
“Tunafarijika kwa msaada huu, kwani mbali na kuimarisha mandhari ya shule, pia utasaidia kupatikana kwa matunda yatakayoongeza lishe kwa wanafunzi wetu. Hii itapunguza magonjwa yanayochangiwa na ukosefu wa virutubisho,” amesema Mwanga.
Amesema shule hiyo imekuwa na utaratibu wa kila mwanafunzi kupanda mti anapojiunga na shule, na hutunukiwa cheti kuthibitisha ushiriki wake.
Mwalimu Maganila Cliford, Mwalimu Mwandamizi wa Idara ya Mazingira shuleni hapo, alisema wamekuwa wakihamasisha wanafunzi kuendelea kutunza miti hiyo hadi wanapohitimu masomo.
“Tunawajengea wanafunzi wetu maadili ya kuwa marafiki wa mazingira. Kupitia utaratibu huu, tunalenga kulea kizazi chenye ari ya kuhifadhi mazingira na kuenzi uoto wa asili,” amesema Cliford.