Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wadau wataka kasi zaidi ufuatiliaji matukio ya watoto kuuawa

Muktasari:

  • Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime atoa ufafanuzi

Dar es Salaam. Wadau na watetezi wa haki za watoto nchini wamesema hawaridhishwi na kasi ya Jeshi la Polisi ya ufuatiliaji wa matukio ya kutekwa, kupotea na kuuawa kwa watoto yanayoendelea.

Wametaka kipaumbele katika uchunguzi wa matukio hayo na umma upewe taarifa sahihi na kwa wakati bila kusubiri kupita saa 24.

Pia, wamemtaka Rais Samia Suluhu Hassan kuendelea kusisitiza ulinzi na usalama wa watoto kwa taasisi zenye mamlaka na ulinzi wa raia kutimiza majukumu yao na kukamilisha uchunguzi haraka kwa matukio yanayojitokeza.

Watetezi hao wameeleza hayo jana Julai 20, 2024, wakati Rais Samia alipozungumza na baadhi ya machifu kutoka mikoa mbalimbali nchini, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, huku akiwataka viongozi hao wa kimila kusaidia kuyazuia matukio hayo kutoka ngazi ya chini.

Akizungumzia kauli ya watetezi hao wa watoto baada ya kutafutwa na Mwananchi, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema Jeshi katika utekelezaji wa majukumu yake hujipima utendaji wake kupitia maoni ya watu, wadau na taasisi mbalimbali.

“Yapo maoni mengine hutolewa ambayo ni chanya na mengine hasi inategemea anayetoa ana taarifa kiasi gani, uelewa kiasi gani na hicho kinachozungumziwa. Yote huwa tunayapokea na kuendelea kuyafanyia kazi endapo yanatusaidia katika utekelezaji wa majukumu yetu ya kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu,” amesema.

Misime amesema matukio yanayohusu watoto yaliyoripotiwa Jeshi la Polisi yanafanyiwa kazi kwa juhudi kubwa usiku na mchana.

“Tunachotaka na kulenga kama Jeshi la Polisi siyo kupambana baada ya matukio kutokea bali kuyabaini na kuyazuia kabla hayajatokea. Hivyo, tutoe wito kwa mtu mmoja mmoja na wadau wengine, sote tuungane na juhudi zinazoendelea za kuzuia yasitokee.”

“Tushirikiane katika kutoa elimu kuanzia ngazi ya familia na katika makundi yote ili sote kwa pamoja tuzuie vitendo hivi viovu ambavyo ni zao la familia kama hakuna malezi bora.

“Pia, tuwe na uelewa wa pamoja kuwa kazi hii ya kuyazuia matendo hayo si kazi ya taasisi moja bali sote kama Watanzania kwa nafasi ya kila mmoja aliyonayo katika jamii.”


Watetezi wa watoto

Wakizungumza jijini Dar es Salaam leo Jumapili  Julai 21, 2024 wakiomboleza vifo vya watoto waliopoteza maisha na kudai ulinzi zaidi kwa watoto, wadau hao wamelaani vitendo vya kutekwa, kupotea, kuibwa na mauaji ya watoto yanayoripotiwa maeneo mbalimbali.

“Tunataka jitihada zifanywe na Serikali na wadau kuwalinda watoto na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakumba. Tunasikitika kuona ukatili kwa watoto unaendelea, tunatoa pole kwa familia zilizokumbwa na kadhia hii kwa kuwa si jambo rahisi kupitia,” amesema Mkurugenzi wa Taasisi ya Genesis, Irene Kitoti.

Amesema pamoja na jitihada zinazofanywa na Jeshi la Polisi bado hawaridhishwi, hivyo wanataka uwajibikaji zaidi kwa chombo hicho kwa kuwa kina mamlaka ya kulinda usalama wa raia.

“Haturidhishwi na kasi ya Jeshi la Polisi katika ufuatiliaji wa matukio ya kutekwa na kupotea, kuuawa kwa watoto yanayoendelea katika nchi yetu,” amesema.

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Wanawake Watetezi wa Haki za Binadamu (CWHRDS), Hilda Dadu amesema matukio hayo yanahusishwa zaidi na masuala ya kisiasa kuelekea uchaguzi.

“Rai yetu sisi watetezi wa haki za watoto tunasema ushindani wa kisiasa hauwezi kushinda kwa sababu ya kutumia viungo vya binadamu,” amesema.

Amesema ushindani wa kisiasa unakuwa na nguvu kwa kujenga hoja na kuwa na ajenda itanayoweza kuleta maendeleo kwa Watanzania.

“Kutumia ushirikina wa viungo vya watoto inaongeza ukatili wa kijinsia na kuwanyima haki za kuishi na haki za upendo, wanakuwa na wasiwasi,” amesema.

Hilda amewataka wanasiasa wenye mtindo huo kuacha dhana hiyo ili kuleta amani kwa jamii inayoendelea kuishi kwa wasiwasi nchini kutokana na kuongezeka kwa matukio hayo.

“Tumepokea matukio saba ya watoto kuuawa na wengine kutekwa likiwamo lile la mkoani Kagera mtoto Asimwe Novart (2) alitekwa akiwa mikononi mwa mama yake na baadaye alikutwa amefariki  dunia na baadhi ya viungo vyake kukosekana,” amesema.

Hilda ametaja baadhi ya matukio hayo ni lililotokea Julai 15 mwaka huu, mkoani Dodoma la mtoto Sumaiya Issa kupotea na mpaka sasa hajapatikana.

Julai 7, 2024 eneo la Mbagala, Dar es Salaam mtoto Nusura Omari alikutwa ameuawa na baadhi ya viungo vyake kunyofolewa.

“Julai 17, 2024 mkoani Dodoma, mtoto Theresphoa Mwakalinga alikutwa amekufa na baadhi ya viungo vyake kunyofolewa baada ya kupotea jioni ya siku hiyo,” amesema.