Waethiopia wadakwa Manyara, gari yakutwa na namba ya Serikali

Muktasari:

  • Wakamatwa Babati wakiwa kwenye gari ambalo mmiliki wake hajabainika.

Babati. Polisi mkoani Manyara inawashikilia Waethiopia 17 wanaodaiwa kuingia nchini bila kibali wakitaka kuelekea Afrika Kusini kupitia mkoani Dodoma.

 Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Aprili 8, 2024 Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Lucas Mwakatundu amesema waethiopia hao wamekamatwa jana Aprili 7 katika mtaa wa Maisaka, mjini Babati wakiwa kwenye gari aina ya Toyota Land Cruiser V8 VXR.

Amesema bado hawajabaini mmiliki wa gari hilo lililokuwa na namba mbili (T723 BSF na STL 1964) na wanaendelea na uchunguzi, ili kumbaini mmiliki.

Amesema waethiopia hao 17 wamekamatwa wakiwa ndani ya gari hilo ambalo waling'oa baadhi ya viti, ili waenee wote.

"Tunatarajia kuwakabidhi kwa Idara ya Uhamiaji waethiopia hao 17 kwa hatua nyingine, ikiwemo kufikishwa mahakamani na kujibu shtaka linalowakabili," amesema Kaimu Kamanda Mwakatundu.

Ametoa wito kwa wana Manyara kutojihusisha na watu wanaoshiriki kusafirisha binadamu kwa lengo la kujipatia kipato, kwani si jambo halali.

"Polisi tumejipanga kuhakikisha hakuna magendo au raia wasio Watanzania watakaopita Manyara bila kuwa na vibali. Tunaomba ushirikiano wa raia, ili kufanikisha," amesema.

Machi 23, 2024 waethiopia 20 walikamatwa eneo la Minjingu mjini Babati wakielekea mkoani Mbeya kupitia Dodoma, lengo likiwa kufika Afrika Kusini.

Hata hivyo, waethiopia hao wameshahukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na miezi sita jela au kulipa faini ya Sh1 milioni kila mmoja.