Wafanyabiashara 100 kushiriki maonyesho Arusha

Katikati ni Mratibu wa maonesho hayo , Augustine Namfua akizu gumza na waandishi wa habari aliyeko kushoto ni Meneja wa Tigo Kanda ya kaskazini,Daniel Mainoya na pembeni ni Meneja huduma kwa wateja kampuni ya Radar Security Ltd Arusha, Aingiki Kileo. Picha na  Happy Lazaro

Muktasari:

Zaidi ya wafanyabiashara100 kutoka mkoani Arusha wanatarajiwa kushiriki kwenye maonesho makubwa ya biashara yatakayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuanzia Desemba 13 hadi 19 mwaka huu.

Arusha. Zaidi ya wafanyabiashara100 kutoka mkoani Arusha wanatarajiwa kushiriki kwenye maonesho makubwa ya biashara yatakayofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuanzia Desemba 13 hadi 19 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo Desemba 6, 2021 Mratibu wa maonesho hayo, Augustine Namfua amesema kuwa, maonesho hayo yanayohusisha biashara mbalimbali yanalenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara wakubwa,wa kati na wafanyabiashara wadogo (wajasiriamali) kujitangaza na kufanya biashara hasa katika kipindi cha msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.

Namfua amesema kuwa, maonesho hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na wananchi zaidi ya 10,000 kwa siku zote za maonesho ambapo wananchi wataweza kujipatia mahitaji yao yote muhimu kimanunuzi kuelekea msimu wa mwisho wa mwaka.

"Kufanyika kwa maonesho haya wiki nzima kunalenga kutoa fursa kwa wafanyabiashara kuwa na muda wa kutosha wa kufanya biashara na vilevile kwa watembeleaji kuwa na muda mrefu zaidi kufanya manunuzi"amesema.

Amesema kuwa, maonesho ya mwaka huu yana utofauti mkubwa kwani  yamepangiliwa kwa mfumo wa mitaa ambapo bidhaa zinazofanana hukaa eneo moja linaloitwa mtaa na kumrahisishia mtembeleaji kujua aina za bidhaa na sehemu ya kuzipata kirahisi.


Naye  Meneja wa Tigo Kanda ya Kaskazini , Daniel Mainoya ambao ndio wadhamini wakuu wa maonesho hayo wakishirikiana na washirika wengine wakiwemo kampuni ya Bulb Africa  amesema kuwa,maonesho hayo yanatoa fursa kwa wafanyabiashara hao kutangaza biashara zao na kuweza kujikwamua kiuchumi hususani msimu huu wa sikukuu.

"Kampuni ya Tigo imekuwa mstari wa mbele katika kubuni bidhaa na huduma zinazowalenga wafanyabiashara moja kwa moja kupitia huduma ya lipa kwa simu ,ambapo mfanyabiashara yoyote atakayekuwa na banda hapo anatumia huduma ya lipa kwa simu huduma ya kifedha ya kidigitali inayomfanya mfanyabiashara au Taasisi kupokea fedha kutoka kwa wateja wanaotumia simu  za mkononi" amesema Mainoya.

Amefafanua kuwa, gharama za maonesho hayo ni 1,000 kwa kulipia huduma ya lipa kwa simu ya Tigo ama Sh2,000 kwa kulipia kwa pesa taslimu mlangoni, hivyo ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Arusha na mikoa jirani kushiriki na kutembelea maonesho ili kujipatia bidhaa na huduma mbalimbali kipindi hiki cha msimu wa sikukuu.

Imeandikwa na Happy Lazaro

Naye Meneja wa huduma kwa wateja kutoka kampuni ya ulinzi ya Radar Security Ltd Arusha, Aingiki Kileo amesema kuwa, wakiwa kama kampuni ya ulinzi watahakikisha ulinzi umeimarishwa kwa siku zote za maonesho.