Wafanyabiashara Mwenge walia kuvunjiwa vibanda

Wafanyabiashara Mwenge walia kuvunjiwa vibanda

Muktasari:

  • Baadhi ya wafanyabiashara wadogo eneo la Mwenge Mlalakua  mkoani Dar es Salaam  wamevunjiwa maeneo yao ya biashara tangu Aprili 25, 2021 na hadi leo Jumamosi Meimosi, 2021 hawajui hatima yao.

Dar es Salaam. Baadhi ya wafanyabiashara wadogo eneo la Mwenge Mlalakua  mkoani Dar es Salaam  wamevunjiwa maeneo yao ya biashara tangu Aprili 25, 2021 na hadi leo Jumamosi Meimosi, 2021 hawajui hatima yao.

Akizungumza na Mwananchi Digital mwenyekiti wa wafanyabiashara hao takribani 15, Revocatus Emmanuel amesema siku ya tukio mwenyekiti wa mtaa alikwenda eneo hilo na kumpa maelekezo ya kuondolewa kwa vibanda hivyo kwa kuwa hakuna kazi inayoendekea eneo hilo.

“Baada ya muda wakaja walioambiwa watoe vibanda, ilikuwa muda wa saa nne asubuhi, walikuja na toroli kwa lengo la kuvisomba vile vibanda. Nikahoji kwa nini mnatoa vibanda  wakati vinafunguliwa? Wakaanza kutumia nguvu kuviondoa,” amesema.

Wini Michael, mama lishe katika eneo hilo amesema amevunjiwa banda lake lote na hajui hatma yake mpaka sasa.

“Nimeanza kufanya biashara hapa tangu mwaka jana mwezi wa kumi na mbili sasa ghafla tu wamekuja wametuvunjia, wakatuambia turudi, jana tena wanatuambia tuondoke. Sasa hatujui hatma ni nini. Mimi familia inanitegemea, tangu nimevunjiwa banda langu mpaka leo sijafanya biashara yaani napata shida sana,” amesema Wini.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mlalakuwa, Suleiman Masare amesema, “kuna maelekezo tulitoa kwamba kuna vibanda viwili ambavyo havifanyi kazi vinatakiwa vitolewe lakini inavyosemekana wakati tunatoa hayo kuna upande mwingine (baa iliyopo jirani) ukawashawishi hao wahuni kwa maslahi yao binafsi kwamba hilo eneo libaki wazi.”