Wafanyabiashara wafunga maduka kisa kupandishiwa kodi

Muktasari:

  • Wafanyabiashara zaidi ya 100 wa maduka katikati ya Jiji la Arusha wamefunga maduka yao bila kikomo wakipinga kupandishiwa mara dufu  kodi na halmashauri ya Jiji la Arusha kutoka Sh150,000 hadi Sh300,000 kinyume na utaratibu.


Arusha. Wafanyabiashara zaidi ya 100 wa maduka katikati ya Jiji la Arusha wamefunga maduka yao bila kikomo wakipinga kupandishiwa mara dufu  kodi na halmashauri ya Jiji la Arusha kutoka Sh150,000 hadi Sh300,000 kinyume na utaratibu.

Aidha wamemwomba Rais Samia Suluhu na Waziri Ummy Mwalimu kuingilia kati ili kuondoa unyanyasaji huo unaosababisha washindwe kufanya biashara zao kwa uhuru.

Wakiongea na waandishi wa habari leo Desemba 10,  wafanyabiashara hao katika eneo la Ranger Safari, wamedai kuwa kitendo cha halmashauri hiyo kupandisha kodi ya pango kinyemela hakikuwa na makubaliano bali halmashauri hiyo imetumia ubabe wakati mwafaka   ulikuwa bado.

Baadhi ya wafanyabiashara hao Godluck Alick na  Amani Mollel wamedai kuwa usiku wa siku ya kusherehekea miaka 60 ya uhuru wa Tanzania ,baadhi ya maofisa wa jiji wakiwa na mgambo kadhaa walivamia katika maduka hayo na kuwakamata viongozi wa wafanyabiashara hao na kuwapelekea polisi wakidai wanashinikiza wafanyabiashara wasilipe Kodi.

"Hili suala lilishazungumziwa na mkuu wa wilaya aliyepita Mbele ya mkurugenzi wa jiji na kufikia mwafaka kwamba wafanyabiashara hao waendeleee kulipa kodi ya zamani ya shilingi laki moja na nusu ,lakini tumeshangaa hapo jana jambo hili limeibuka upya"alisema Mollel.

Naye mwenyekiti wa Jumuiya ya wafanyabiashara hao,Loken Masawe na Katibu wake,Hamidur Jamari wamemwomba Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kukaa na Wafanyabiashara hao ili kuondoa sintofahamu inayojitokez kwa kuwa msuguano huo umekuwa wa muda mrefu unaosababisha adha kwa wananchi.

"Hawa wafanyabiashara ndio waliojenga haya maduka wanamchagia wao ni mkubwa kwa Serikali. Huyu mkurugenzi akutane na wafanyabiashara na awaheshimu kwa mchango wao kitendo cha kuwatumia mgambo siku ya uhuru na kuwakamata viongozi wao awaombe radhi sio cha uungwana"alisema Masawe.


Aidha mwenyekiti huyo amedai kuwa wafanyabiashara hao hawatafungua maduka yao katika muda usiojulikana ili kushinikiza halmashauri hiyo kukaa kitako ili kufikia mwafaka.

Katika hatua nyingine wafanyabiashara waliopanga katika maduka mapya ya halmashauri hiyo yaliyopo eneo la Disemba nao wamegoma kufungua wakidai kiwango cha kodi wanachoyozwa na halmashauri hiyo ni kikubwa.

Mmoja ya wapangaji wa maduka hayo, Modester Kapinga alidai kuwa kodi wanayolipa kwa sasa ni kati ya ya Sh,300,000 na Sh600,000, ambayo haiwapi faida na kwamba maduka hayo ni madogo sana..

Akijibu hoja za wafanyabiashara hao mstahiki meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iranghe alisema uamuzi wa kupandisha Kodi ni uamuzi uliotolewa na baraza la madiwani baada ya kujiridhisha kuwa wafanyabiashara hao wanalipwa kiasi kidogo cha kodi .

"Haya maamuzi yametolewa na baraza la madiwani halmashauri ni watekelezaji tu, hao wafanyabiashara wanalipa kodi ndogo sana"alisema Meya.

Awali mkurugenzi wa Jiji la Arusha,Dkt John Pima alidai kuwa suala hilo litazungumziwa na Meya wa Jiji la Arusha kwa sababu maamuzi ya kupandisha kodi yalifikiwa na baraza lake la madiwani.

Imeandikwa na Teddy Kilanga Mwananchi