Wafugaji 69,000 waula kupitia mradi wa uzalishaji, usindikaji maziwa
Muktasari:
- Mradi huo wa miaka minne unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Taasisi ya Mfuko wa Bill and Melinda Gates na kutekelezwa na Heifer International, Land O’Lakes Venture 37, pamoja na Tanager.
Mwanza. Jumla ya wafugaji wadogo 69,062 kutoka maeneo mbalimbali nchini, wamenufaika na mradi shirikishi wa wasindikaji na wazalishaji wa maziwa (TI3P) uliozinduliwa Machi 2022.Mradi huo wa miaka minne unafadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kushirikiana na Mfuko wa Bill and Melinda Gates na kutekelezwa na Heifer International, Land O’Lakes Venture 37, pamoja na Tanager.Akizungumza leo Jumapili, Juni 2, 2024 katika maonyesho ya 27 ya wiki ya maziwa jijini Mwanza, Meneja wa TADB Kanda ya Ziwa, Alphonce Mokoki amesema mradi huo unalenga kutatua changamoto mbalimbali kwenye mnyororo wa thamani wa sekta ndogo ya maziwa ili kuongeza kipato cha wafugaji wadogo. “Mradi wa TI3P unalenga kuongeza upatikanaji wa maziwa na ukuaji wa sekta hii kwa ujumla, ili kuwaongezea faida wasindikaji ambao ndiyo soko kuu la maziwa yanayozalishwa na wafugaji wadogo,” amesema Mokoki.Amesema tangu mradi huo uanze, wasindikaji sita wameshiriki katika programu ya kujengewa uwezo ambayo imesaidia kuongeza uzalishaji kwa asilimia 17.Meneja huyo amesema TADB kwa kushirikiana na washirika wa mradi huo, wamefanikiwa kuwafikia wafugaji wadogo 69,062 ambao wamepatiwa huduma za ughani, pembejeo, masoko na mikopo kwenye eneo zima la mnyororo wa thamani katika sekta ndogo ya maziwa.“Kupitia mradi huu, jumla ya mikopo yenye thamani ya Sh26 bilioni imetolewa kwa wasindikaji, wafugaji wadogo, watoa huduma za ughani na wadau wengine waliopo kwenye mnyororo wa thamani. TADB pia imetoa Sh738 milioni kama ruzuku kwa wakulima wadogo 846,” amesema Mokoki.Jumla ya vyama vya ushirika 45 na vikundi 888 vyenye masilahi katika sekta ya maziwa vyenye wanachama 20,612 vimeundwa na kuimarishwa, na sasa vinakusanya lita 15,000 kwa siku.Mokoki amesema TADB ipo kwenye hatua ya mwisho ya kuanzisha vituo 15 vya kukusanyia maziwa kwenye mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, na Shinyanga.Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Daniel Mushi amewataka wafugaji nchini kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na TADB, ikiwa ni pamoja na mikopo yenye riba nafuu.