Wafungwa wanaosubiri kunyongwa watuma salamu kwa Rais Samia

Wafungwa wanaosubiri kunyongwa watuma salamu kwa Rais Samia

Muktasari:

  • Wafungwa 69 wanaosubiri adhabu ya kunyongwa hadi kufa wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan awape adhabu mbadala.

  

Tabora. Wafungwa 69 wanaosubiri adhabu ya kunyongwa hadi kufa wamemwomba Rais Samia Suluhu Hassan awape adhabu mbadala.

Wafungwa hao waliopo gereza kuu la Uyui mkoani hapa, walitoa ombi hilo kupitia risala yao iliyosomwa mbele ya makatibu wakuu watatu wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome.

Akisoma risala hiyo kwa niaba ya wafungwa wenzake, mfungwa kiongozi Masali Misalaba alimuomba Rais Samia awabadilishie adhabu ili waweze kufanya kazi kama ilivyo kwa wafungwa wengine.

“Sisi wafungwa tuliohukumiwa kunyongwa, tunakuomba utufikishie ombi letu kwa Rais Samia atuonee huruma na atupunguzie adhabu hii, ili nasi tuweze kufanya kazi. Tuna wakati mgumu na tunawasumbua askari magereza,” alisema Misalaba.

Wafungwa hao walipewa nafasi na uongozi wa gereza kujumuika na mahabusu na wafungwa wenzao katika kikao hicho ambacho walipata fursa ya kuelezea changamoto zinazowakabili.

Mbali na wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, mahabusu na wafungwa wengine nao waliiomba Serikali kuangalia upya utaratibu wa msamaha wa wafungwa unaotolewa na Rais.

Katika risala yao iliyosomwa na mfungwa, Enock Ezekiel Kakamba walipendekeza wigo wa msamaha unaotolewa na Rais upanuliwe zaidi na kuwahusisha pia wafungwa ambao wametumikia vifungo virefu vya zaidi ya miaka 10.

“Tunaomba msamaha wa Rais ikiwezekana uhusishe pia wafungwa waliotumikia vifungo vyao kwa zaidi ya miaka 10 na kuonyesha tabia njema.

“Tunaomba hivi kwa sababu msamaha ambao umekuwa ukitolewa kwa wafungwa ambao hawajatumikia vifungo muda mrefu, wakishaachiwa baada ya muda mfupi wanarejea gerezani kwa sababu muda waliokaa wanakuwa hawajajifunza chochote tofauti na mfungwa aliyetumikia zaidi ya miaka 10 huyu anakuwa ameshajifunza na hatatamani kurudi tena gerezani,” alisema.

Pia, mahabusu hao wameomba kushughulikiwa kwa suala la uchelewesheaji wa upelelezi, uchelewaji wa kutolewa kwa nakala ya hukumu kwa wakati, uchache wa vikao maalumu vya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani hasa kwa kesi za mauaji na kesi za uhujumu uchumi.

Pamoja na hayo, wameomba sheria ya Parole iangaliwe upya, ili kuwa na wigo mpana tofauti na ulivyo hivi sasa ambapo ina wigo mfinyu katika makosa na muda.

Akijibu ombi la wafungwa waliohukumiwa kunyongwa, Katibu Mkuu, Profesa Mchome, alisema atalifikisha ombi hilo kwa mamlaka zinazohusika.

Mkuu wa gereza hilo, ACP Mussa Said Mkisi, alisema gereza lina wafungwa na mahabusu 767. Idadi hiyo ikijumuisha wahalifu ambao si raia wa Tanzania kutoka nchi za Burundi, Kongo (DRC) na Ethiopia.

Mkisi alisema msongamano wa wafungwa na mahabusu ni wa wastani. “Gereza lina msongano wa wastani wa wahalifu 767 wakati uwezo wa gereza ni kuhifadhi wafungwa na mahabusu 650. Ziada ni wahalifu 117 sawa na asilimia 18,” alisema Mkisi.

Makatibu wakuu wanaongozana na Profesa Mchome ni John Jingu(Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) na Christopher Kadio (Mambo ya Ndani) wapo katika ziara ya kujifunza na kufanya tathimini kuhusu mnyororo wa utoaji haki jinai na haki madai katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Kagera.