Wagonjwa wadai hununua dawa maduka binafsi

Muktasari:
Muuguzi mkuu wa zamu amesema dawa zote muhimu zipo lakini upungufu unajitokeza kwenye dawa maalumu.
Dar es Salaam. Licha ya Serikali kuongeza bajeti ya dawa, wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Amana wilayani Ilala wamesema bado wananunua kwenye maduka binafsi.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu akijibu swali bungeni wiki hii, alisema Serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka Sh30 bilioni mwaka 2015 hadi Sh261 bilioni mwaka huu 2017/18 ikilenga kumaliza ukosefu wa dawa kwenye hospitali nchini.
Hata hivyo, leo Jumamosi Novemba 11,2017 imebainika kuwa katika Hospitali ya Amana bado kuna wagonjwa wananunua dawa katika maduka binafsi.
Hayo yamebainika wakati wanafunzi wa Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (DSJ) walipokwenda hospitalini hapo kutoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh1.4 milioni.
Vifaa tiba hivyo ni pamoja na mashine ya kutolea taka mwili yenye thamani ya Sh280,000 . Kwa msaada huo hospitali hiyo sasa itakuwa na mashine tatu za aina hiyo.
Siwajibu Mipango aliyekuwa hospitalini hapo amesema licha ya huduma kuimarika bado hawapati dawa na kulazimika kununua kwa gharama kubwa.
"Tangu nimefika hapa juzi naandikiwa dawa lakini wananiambia nikanunue," amesema
Elias Ndakuka ambaye alikuwa hospitalini hapo pia.
Akizungumzia hali hiyo, muuguzi mkuu wa zamu, Theresia Akidda amesema dawa zote muhimu zipo lakini upungufu unajitokeza kwenye dawa maalumu.
Kuhusu vifaa tiba amesema bado vinahitajika na hasa kwa ajili ya wazazi.
Mratibu wa masomo wa DSJ, Joyce Mbogo amesema msaada walioutoa ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha huduma za afya.