Wahitimu OUT wahimizwa kuchochea mabadiliko ya mitaala

Muktasari:

  • Wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) wametakiwa kuchochea mabadiliko ya mitaala nchini humo ili mfumo wa elimu ulete tija na suluhisho katika changamoto zinazoikabili jamii ya Watanzania.

Dar es Salaam. Wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) wametakiwa kuchochea mabadiliko ya mitaala nchini humo ili mfumo wa elimu ulete tija na suluhisho katika changamoto zinazoikabili jamii ya Watanzania.

Hayo yamebainishwa leo Alhamisi Septemba 22, 2022 na waziri wa zamani, Mudhihir Mudhihir wakati wa mkutano mkuu wa chama cha wahitimu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).

Mudhihir amesema kuna haja ya kuangalia upya mitaala ya elimu hapa nchini ili iendane na wakati na kutatua changamoto za wananchi kwa njia rahisi na teknolojia ya Kitanzania.

Amesema vyuo vya Tanzania vinazalisha wahandisi wa kutosha lakini wakulima wa korosho wananunua mashine za kubangulia korosho kutoka Vietnam na Uturuki wakati zingeweza kutengenezwa hapa nchini.

"Alumni tunayo nafasi ya kuwasaidia watunga sera kufanya mabadiliko ya mitaala yetu ili iendane na wakati. Wajibu wa alumni sio tu kuwajibika kwenye chama chake, bali pia kuchochea mabadiliko katika jamii," amesema Mudhihir ambaye pia ni mhitimu katika chuo hicho.

Amesema tangu Tanzania imepata uhuru mwaka 1961, mfumo wa elimu haujabadilika, hivyo amesisitiza kuna haja ya kuchochea mabadiliko hayo hasa kwa kutoa elimu ya ujuzi kwa wanafunzi.

Awali, Rais wa wahitimu wa chuo hicho, Almasi Maige amesema wahitimu wanatakiwa kuwa karibu na chama chao ili kukisaidia chuo lakini pia kunufaika na fursa mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho.

"Sisi wanachama tuna fursa ambazo tunazipata kwa kushirikiana na chuo. Kwa hiyo tunaunganishwa na chuo hiki na kimetusaidia wengi kutimiza ndoto zetu," amesema Maige