Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waiangukia Serikali punguzo bei  nyumba za watumishi wa umma

Muonekano wa nyumba moja kati ya 59 zilijengwa Kijiji cha Isangijo Kata ya Bukandwe wilayani na Watumishi Housing Investments(WHI) kwaajili ya kuuziwa watumishi wa umma mkoani Mwanza. Picha na Saada Amir

Muktasari:

  • Katika Kijiji cha Isangijo mkoani Mwanza, nyumba za Watumishi Housing Investments zilizojengwa kwa ajili ya kuwauzia watumishi wa umma zinauzwa kati ya Sh52 milioni hadi Sh82 milioni kulingana na idadi ya vyumba na ukubwa.

Mwanza. Serikali imeombwa kupunguza bei ya nyumba kwaajili ya watumishi wa umma zilizojengwa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza na Watumishi Housing Investments (WHI), zinauzwa Sh52 milioni nyumba ya vyumba viwili na Sh82 milioni nyumba ya vyumba vitatu.

Nyumba hizo 59 zilijengwa Kijiji cha Isangijo Kata ya Bukandwe wilayani Magu katika mwaka wa fedha 2015/16 na kukamilika mwaka 2018 kwa gharama ya Sh3.9 bilioni ikiwa ni mradi wa kuwauzia makazi watumishi wa umma.

Hata hivyo, kati ya nyumba hizo, 20 zimeuzwa huku 39 zikipangishwa kinyume na malengo sababu ikidaiwa bei yake haiendani na kipato cha walengwa wa eneo hilo.

Akizungumza leo Ijumaa Mei 24, 2024 wakati wa ziara ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ya kukagua mradi wa nyumba hizo, Diwani wa Bukandwe, Marco Minzi ameiomba Serikali ipunguze gharama hizo akidai haziendani na uchumi  wa wananchi wa eneo hilo.

“Gharama hizi nyumba kama kutakuwa na uwezekano wa kuzipunguza gharama zake zipunguzwe, kwa gharama ambazo mimi najua ni Sh82 milioni,”amesema Minzi.

Huku akidai bei hizo ni pamoja na kodi ya ongezeko la thamani (VAT), Mkurugenzi Mtendaji wa Watumishi Housing, Fred Msemwa amesema wamesikia maombi ya wateja wao na tayari wanayafanyia kazi.

“Waziri ametoa maelekezo na pia tuna maelekezo ya bodi kwa maana ya kufanya marejeo ya bei ili tukokotoe bei ambazo zitaweza kuedana na hali halisi ya kipato cha watu wa hapa na hivyo kufanya malengo makubwa ya mradi kufanikiwa,” amesema.

Amesema kwa kuwa nyumba 39 hazijauzwa, wamezipangisha kwa watumishi wa umma na binafsi kwa kodi ya Sh150,000, Sh200,000 na Sh250,000 kwa mwezi kulingana na idadi ya vyumba na ukubwa wake.

“Changamoto kubwa ya hii project (mradi) ilikuwa ni gharama ya miundombinu hapa tulilazimika kutengeneza barabara, kuleta maji, kuchimba miundombinu ya kisima pamoja na umeme zote zikawa zimeingizwa kwenye nyumba ukizingatia kwamba tulimtumia mkandarasi badala ya kujenga sisi wenyewe,”amesema

Naye, Waziri Simbachawene amewashauri kujenga nyumba bora kwa gharama nafuu zitakazo mfanya mtumishi wa umma amudu kuzinunua.

 “Mimi maelekezo yangu ni kwamba msingi mkubwa wa Watumishi Housing ni kujenga nyumba kwa ajili ya watumishi, msihame kwenye hiyo sera kwa sababu nyinyi mnaenda mahali ambapo watumishi wana changamoto, mnaweka nyumba ili waweze kununua, kama hamtaliangalia hilo maana yake mtatoka kabisa kwenye mahitaji mtakuwa kama mashirika mengine yanayojenga nyumba kwaajili ya kupangisha,” amesema na kuongeza;

“Ninyi msijifanye kama National Housing (Shirika la nyumba za Taifa), msijifanye kama TBA (Wakala wa Majengo Tanzania), ninyi mnatakiwa mjenge nyumba za bei ndogo ambazo watanunua watumishi ambao mishahara yao mnaijua. Msifikirie sana kibiashara badala yake kutoa huduma bila kupata hasara,” amesema.