Waitara apata pigo kesi ya kumkashfu Maswi

Muktasari:
- Maswi amemfungulia Waitara na wenzake kesi ya kashfa na wadaiwa hao hawakuwasilisha mahakamani kwa wakati maelezo yao ya utetezi ndani ya muda na wamekataliwa kuongezewa fura ya kuwasilisha utetezi.
Dar es Salaam. Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara amepata pigo baada ya Mahakama Kuu Musoma kumfungia milango ya kujitetea yeye na wenzake wawili, katika kesi ya kashfa inayomkabili, iliyofunguliwa na Eliakimu Maswi, mtendaji mkuu wa Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA).
Mahakama hiyo imewafungia milango ya kujitetea kutokana na kushindwa kuwasilisha mahakamani majibu ya madai ya Maswi kwa kuwasilisha maelezo ya utetezi wa awali, kwa njia ya maandishi kabla ya usikilizwaji wa kesi hiyo, ndani ya muda unaotakiwa kisheria wa siku 21.
Mahakama imefikia uamuzi huo baada ya Maswi kupitia wakili wake Kassim Gilla kupinga maombi ya kutaka kuongezewa muda wa kuwasilisha majibu yao, kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.
Katika uamuzi huo uliotolewa jana Machi 19, 2024, Jaji Marlin Komba amewakatalia maombi hayo na kukubaliana na sababu za pingamizi la Wakili Gilla, kuwa hata muda ambao walipaswa kuomba kuwasilisha majibu yao nje ya muda ulishapita.
Amesema baada ya kupitia hoja za pande zote, ni dhahiri wadaiwa walishindwa kutekeleza amri ya mahakama (kuwasilisha majibu yao ndani ya siku 21).
Amesema wadaiwa walipaswa watoe sababu za kuridhisha za kuchelewa kuwasilisha majibu yao ndani ya siku 21 au ndani ya siku saba baada ya kuisha siku 21 za awali, lakini mpaka sasa ni miezi minne hawajafanya hivyo.
Jaji Komba amesema mahakama ilizingatia Katiba ya nchi kuwapa wadaawa haki ya kusikilizwa katika kesi yao…hawakutaka kutumia haki yao ya Kikatiba iliyotolewa na mahakama,” amesema Jaji Komba na kuhitimisha:
“Kwa kutambua hilo, ninayakataa maombi ya mdaiwa wa kwanza na wa pili kwa kuwa yamewasilishwa nje ya muda wa siku saba, hivyo mahakama hii inakosa mamlaka yanayohitajika (kuyakubali) na kesi inapaswa kuendelea kwa mujibu wa sheria dhidi ya mdaiwa wa kwanza na wa pili.”
Kwa hiyo uamuzi huo kina Waitara hawatapata fursa ya kujitetea katika kesi hiyo, itasikilizwa na kuamuriwa upande mmoja.
Maswi amemfungulia kesi hiyo Waitara pamoja na wenzake wawili, Karoli Jacob Karoli na Mara TV, akiiomba mahakama hiyo iwaamuru wamlipe fidia ya Sh13 bilioni kwa madai ya kumkashfu.
Katika hati ya madai, Maswi aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini anadai kuwa Agosti 9, 2023, Waitara aliandaa mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na zaidi ya watu 500 katika Kijiji cha Mtana, Kata ya Manga wilayani Tarime na kutoa maneno ya kashfa dhidi yake.
Anadai katika mkutano huo, alisema Maswi anahusika na anawajibika kwa vitendo vya rushwa kwa matumizi mabaya ya nafasi yake kama mtumishi wa umma katika nafasi ya mtendaji mkuu wa PPRA.
Anadai kuwa Agosti 10, 2023, kwa kushirikiana na Waitara, Karoli na Mara TV waliandaa, wakapakia na kuchapisha katika televisheni ya mtandaoni katika chaneli ya Youtube iitwayo Mara TV, maneno hayo ya kashfa dhidi yake.
Pia Maswa anadai kuwa Agosti 13, 2023, chapisho la maneno hayo yaliyorushwa na televisheni hiyo ya mtandaoni lilikuwa limetazamwa na watu 280 wa aina tofautitofauti kutoka duniani kote.
Anadai kuwa maneno hayo ya kashfa si tu kwamba ni ya uwongo na yana nia ovu, pia hayana msingi na yanalenga kushusha hadhi yake.
Hivyo anawataka wadaiwa wamuombe radhi kwa namna ambayo maneno hayo yalichapishwa, watoe malipo ya Sh12 bilioni kama fidia ya madhara ya jumla aliyoyapata na malipo ya Sh1 bilioni kama fidia ya adhabu.
Wadai hao walitakiwa kuwasilisha majibu yao ya utetezi ndani ya siku 21 tangu walipopewa hati za wito wa mahakama lakini mpaka Machi 13, 2024 kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji, walikuwa hawajayawasilisha.
Wakili wa Waitara, Hekima Mwasipu alidai kuwa alipewa na Waitara jukumu la kumwakilisha Januari 23, 2024, siku 21 zikiwa tayari zimepita, hivyo aliomba kuongezwa muda wa siku tano kuwasilisha majibu.
Wakili wa Karoli, Paul Boman alidai kuwa mteja wake alichelewa kupata msaada wa uwakilishi mpaka Februari 2024, alipopewa kazi hiyo na Baraza la Habari Tanzania (MCT) na mwenzake Ernest Mhagama akipewa kazi hiyo na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) Novemba 17, 2024.
Alidai kuwa ni haki ya kikatiba kujitetea na kwamba mteja wao (Kalori) ni mtu wa kaiwada asiye na uelewa wa masuala ya kisheria na hivyo anaamini ana haki ya kuwakilishwa na kwamba hakuwa mzembe, jambo ambalo lilipingwa na upande wa madai.