Wajasiriamali 1,500 wajengewa uwezo Singida

Muktasari:

  • Wajasirimali 1,500 kutoka halmashauri mbalimbali za mkoa wa Singida zikiwemo za Mkalama, Manyoni na Itigi wapigwa msasa kuhusu usimamizi wa biadhara na usindikaji wa mazao.

Dar es Salaam. Shirika lisilo la kiserikali la Star Entrepreneur General likishirikiana na mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, limetoa mafunzo kwa wajasiriamali katika wilaya zote za mkoa kuhusu namna ya kuendesha biashara zao kwa ufanisi na weledi ili kujikwamua kiuchumi.

Mafunzo hayo ambayo yalianza  Oktoba 3, 2023 yalihitimishwa juzi Novemba 17, 2023 kwa awamu ya kwanza na kwamba  yatakuwa endelevu .Katika awamu hiyo ya kwanza jumla ya  wajasiriamali 1,500 wamenufaika na mafunzo kutoka halmashauri za wilaya za Manyoni, Itigi, Mkalama,Iramba,Ikungi,Singida na  nanispaa ya Singida.

Meneja wa shirika hilo,Yoel Mwenda akitoa taarifa wakati wa kufunga mafunzo hayo amesema wajasiriamali walifundishwa ufugaji wa kuku, kilimo biashara, usimamizi wa biashara, usindikaji wa mazao ya nafaka, mbogamboga na matunda pamoja na utengenezaji wa sabuni,  za miche, utengenezaji wa batiki na utafutaji wa masoko.

Naye, Mattembe amesema ambaye amefadhili mafunzo hayo ameziomba halmashauri zote mkoani Singida kutoa kipaumbele cha kuwapatia mikopo ya kuendeshea biashara zao wajasiriamali waliopata mafunzo ya ujasiriamali.

Mattembe amesema atafanya utaratibu wa kuonana na taasisi zingine za fedha zinazotoa mikopo ili kuangalia uwezekano wa kutoa mikopo kwa wajasiriamali ili kukuza biashara zao na kujikwamua na umaskini, hatimaye kupiga hatua moja kwenda nyingine.

"Nataka kuona mwanamke wa Singida anayepika mandazi na vitumbua anamiliki kiwanda cha kuokea mikate, nataka kuona wanawake  wa Singida wakimiliki migahawa mikubwa na wakimiliki viwanda vikubwa vya kukamua mafuta ya alizeti, inawezekana kabisa.

"Mafunzo hayo yatakuwa endelevu na kila mwaka yatakuwa yakifanyika katika wilaya zote lengo likiwa ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuona kila Mtanzania anakuwa na shughuli ya kujiongezea kipato,"

Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida, Naima Chondo aliyemwakilisha  Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema mafunzo hayo ni  muhimu  hasa  wakati huu ambao Serikali inawekeza kwenye viwanda na wajasiriamali.

Amesema Rais Samia kwa kutambua umuhimu wa wanawake katika kukuza uchumi wa mtu mmoja, jamii na Taifa ameondoa riba katika mikopo wanayokopeshwa wanawake kwa ajili ya kuanzisha shughuli za ujasiriamali.