Wajasiriamali Zanzibar kupigwa jeki

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara (TCB), Adam Mihayo (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi (ZEEA), Juma Burhan wakisaini mkataba wa ushirikiano wa kibiashara baina ya Benki ya TCB na ZEEA kuwasaidia Vijana, Wanawake na Makundi maalum. Aliyesimama Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha huduma za Sheria ZEEA, Maria Malila, Katibu Mkuu Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Zanzibar, Maryam Abdullah Sadala na Mkurugenzi wa Sheria na Karani wa Kampuni, Mystica Ngongi.
Muktasari:
- Wajasiriamali hao watapewa mikopo ambayo itasaidia kupanua biashara zao, kutengeneza fursa mpya za ajira, na hivyo kupunguza uhaba wa ajira.
Dar es Salaam. Ili kuchochea ukuaji wa biashara, ongezeko la ajira, na maendeleo ya kiuchumi Wakala wa uwezeshaji wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA) umeangia makubaliano na Benki ya Biashara Tanzania (TCB) ili kuwezesha vikundi 75 vya wajasiriamali.
Ili kutimiza lengo hilo ZEEA na TCB zimesaini mkataba wa makubaliano ya kimkakati yanalenga kuanzisha mpango maalum wa mikopo utakaonufaisha makundi maalum, wakiwemo wanawake na vijana wanaojihusisha na shughuli za kiuchumi visiwani Zanzibar.
Malengo ni kuvifikia vikundi 75 vyenye wanachama kati ya watano mpaka 20. Mpaka sasa ZEEA imeshasajili vikundi 16 kutoka sekta muhimu na kupokea maombi ya mkopo yanayofikia wastani wa Sh150 milioni.
Kwa makubaliano haya na TCB sasa yataviwezesha vikundi hivi kupokea mikopo nafuu inayofikia kiasi cha Sh30 milioni kwa kikundi, huku wakipewa muda miezi 24 sawa na miaka miwili kurejesha.
“Tuna furaha kushirikiana na ZEEA kuwainua wajasiriamali wanawake, vijana na makundi mengine maalum yaliyomo visiwani Zanzibar,” amesema Adam Mihayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB.
Ameongeza: “Mpango huu unaendana na lengo letu la kuwezesha maendeleo ya kiuchumi kwa kujenga uchumi jumuishi. Kwa kuyawezesha makundi maalum, tunaziinua biashara binafsi, pamoja na kuimarisha mfumo mzima wa uchumi na kutengeneza mazingira imara ya kiuchumi.”
Mihayo anasema malengo ya uwezeshaji huu ni kuwa chanzo cha mabadiliko mengine kama kuimarisha uchumi wa ndani, kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupambana na ukosefu wa ajira na kuleta maendeleo.