Wakala za Serikali zalia na mfumo wa ajira, Serikali yajibu

Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Menejinent ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene (Picha na Mtandao)
Muktasari:
- Wakala za Serikali zimetaka ama zipewe nafasi ya kuajiri zenyewe au jukumu la kufanya hivyo likasimikwe kwao.
Dar es Salaam. Mfumo wa sasa wa kuajiri kupitia sektretarieti ya ajira ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa na Wakala za Serikali kuwa kikwazo cha kutimiza malengo ya kuanzishwa kwao.
Zimesema ili zifikie malengo hayo ni vema ama zipewe nafasi ya kuajiri zenyewe au jukumu ya kuajiri likasimikwe kutoka mamlaka husika kwenda kwao.
Hoja hiyo imewasilishwa leo Alhamisi Julai 27, 2023 na Mkuu wa Chuo cha Kodi, Dk Tumaini Katunzi aliyezungumza kuwakilisha Wakuu wa wakala hizo katika mkutano wa Wakala za Serikali jijini Dar es Salaam.
Dk Katunzi amesema pendekezo hilo linatokana na mfumo wa ajira, huajiri taaluma ambazo wakati mwingine ni kinyume na zinazohitajika na wakala hizo.
"Bado mfumo wa ajira haukidhi uendeshaji wa wakala kwa maana tuna mahitaji tofauti, zipo zinazotoa huduma na zile zinazofanya biashara, ili ziendeshwe kwa ufanisi zinahitaji aina ya watu watakaofanya kazi kwenye wakala hizo," amesema.
Kwa sababu taaluma inayohitajika inajulikana na wakala husika, amesema ni vema wapewe mamlaka ya kuajiri au jukumu hilo likasimiwe kwao.
"Sisi ndiyo tunaojua taaluma tunazozihitaji kuna haja ya kupewa nafasi ya kuajiri au kukasimiwa jukumu hilo," amesema.
Akijibu hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema mfumo uliopo unatoa nafasi hiyo.
Amesema sektretarieti ya ajira inaajiri kwa kupewa vigezo vya taaluma inayohitajika na wakala za Serikali, haiamui yenyewe kuchagua.
"Uchaguzi wa vigezo vya waajiriwa vinatoka kwenu, mnahusishwa hadi kwenye usaili na kila eneo, asilimia 85 ya vigezo vya waajiriwa vinatoka kwenu sasa sioni sababu ya mnachohitaji," amesema.
Simbachawene amesema Serikali ilibadilisha utaratibu huo kuondoa changamoto zilizokuwepo, ikiwemo nafasi kutolewa kwa upendeleo.
"Hivi leo ukipewa nafasi ya kuajiri wewe ndiyo Mtendaji Mkuu wa taasisi, lazima utatoa upendelea kwa watu fulani.
"Fikiria mimi Waziri kwa sasa ndiyo nina wageni wengi kwangu kuliko wakati wowote wanaomba ajira, sasa ndiyo nipewe nafasi ya kuajiri nitaacha kupendelea? Ndiyo maana tulitoka huku," amesema.
Maeneo mengine yaliyopendekezwa kuboresha ufanisi wa wakala za Serikali kwa mujibu wa Dk Katunzi ni ukinzaji wa majukumu.
Amesema bado baadhi ya wakala na Wizara zinagongana kwa majukumu haijulikani nani atekeleze lipi na aache lipi kwa mwingine.
Mapendekezo mengine ni kuangalia namna ya kuzipa motisha na nyongeza ya mishahara, kadhalika kuwezeshwa miundombinu ya kazi.
Kuhusu motisha na mishahara, Simbachawene amesema ni muhimu nchi kuwa na mfumo mmoja ili kuleta uwiano kwa wote.
"Kila Mkurugenzi anapambania watumishi wa taasisi yake waongezewe mshahara, hivi mmewafikiria walimu na wauguzi huko, wote tuwe kwenye skimu Sawa ili kutoa haki kwa wote," amesema.