Wakamatwa na kilo 23 za meno ya tembo

Friday November 27 2020
By Florah Temba

Moshi. Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linawashikilia watu wawili wakazi wa Rombo kwa tuhuma za kukutwa na vipande  10 vya meno ya tembo yenye uzito wa Kilogramu 23.

Akitoa taarifa ya kukamatwa kwa  nyara hizo za serikali leo Ijumaa Novemba 27, 2020 kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Emmanuel Lukula amesema watu hao walikamatwa Novemba 25  saa 5:30 asubuhi katika kijiji cha  Kikelelwa wilayani Rombo.

Amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Nicholaus Kimari (53) na Christian Tarimo (56) wakazi wa kijiji cha Kikelelwa na kwamba kulingana na meno hayo, ni wastani wa tembo wanne wameuawa.

Amebainisha kuwa kukamatwa kwa watu hao kumetokana na taarifa za siri zilizopatikana kuwa wanashirikiana na kundi la majangili kutoka nchi jirani kufanya biashara ya meno ya tembo.

“Jeshi la polisi kwa kushirikiana na kikosi kazi cha kuzuia na kupambana na ujangili  kanda ya Kaskazini, tulifanikiwa kuwakamata watu wawili baada ya kupata taarifa ya siri kuwa wanashirikiana na kundi la majangili kutoka nchi jirani, wanafanya biashara ya kuingiza na kuuza meno ya tembo nchini kwetu," amesema Lukula akisisitiza kuwa wanaendelea kuwafuatilia wengine.


Advertisement
Advertisement