Wakazi 10,000 wapata huduma ya maji Musoma vijijini

Muktasari:
Wakazi zaidi ya 10,000 wa vijiji vya Makojo, Chitare na Chimati katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara wameondokana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama baada ya mradi wa maji ya bomba uliojengwa kwa miaka tisa kukamilika.
Musoma. Wakazi zaidi ya 10,000 wa vijiji vya Makojo, Chitare na Chimati katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara wameondokana na tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama baada ya mradi wa maji ya bomba uliojengwa kwa miaka tisa kukamilika.
Akitoa taarifa ya mradi huo leo Jumatano Aprili 26, 2023, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) wilayani Musoma, Edward Sironga amesema mradi huo ulioanza kujengwa 2014 katika kijiji cha Makojo kwa gharama ya Sh1.07 bilioni.
“Wakazi wa kijiji cha Chitare tayari wameanza kutumia maji ya bomba na leo wakazi wa kijiji hiki cha Makojo wataanza kunufaika na maji ya mradi wakati tunamalizia upanuzi wa mradi kwa kijiji cha Chimati ili nao wapate huduma ya maji safi,”amesema Sironga
Akizindua mradi huo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Suleiman Mzee amesema Serikali imedhamiria kwa dhati kupunguza na kumaliza kabisa tatizo la ukosefu wa maji kwa wananchi na kuzitaka mamlaka husika kuhakikisha kuwa wananchi wanahamasishwa kuunganisha huduma mara tu mradi unapokamilka.
“Miradi hii ili iweze kuwa endelevu ni lazima watumiaji wawe wengi niwaombe muwe wabunifu mnaweza hata kuwaunganishia maji wateja kwa mkopo kisha wakawa wanalipa taratibu na hii itafanya miradi kuwa na tija na sio mradi unakufa kwa kukosa hela ya uendeshaji,”amesema
Amesema jumla ya miradi 52 ya maji yenye thamani ya zaidi ya Sh15.7 bilioni imetekelezwa mkoani humo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita huku miradi 42 yenye thamani ya zaidi ya Sh13.3 bilioni ikiendelea kutekelezwa mkoani humo ambayo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mkazi wa kijiji cha Makojo, Nyanjura Chimwejo amesema kukamilika kwa mradi huo ni nafuu katika maisha yao kwani walikuwa wanatumia muda mrefu kufuata maji ziwani licha ya kijiji chao kuwa jirani na Ziwa Victoria.