Wakazi wa Buza walalamika usalama wa mazingira yao

Baadhi ya takataka zilizotelekezwa katika mtaa wa Buza Newstime, picha na Emmanueli Msabaha
Muktasari:
- Wananchi wa Buza walalamikia uongozi wa mtaa kwa kutokuweka mazingira rafiki, hali ambayo inawasababisha kuwa na wasiwasi huenda wakakumbana na magonjwa ya mlipuko kama Kipindupindu.
Dar es Salaam. Wakazi wa Buza wameulalamikia uongozi wa Mtaa wa amani, kwa kutokuweka mazingira salama, hali ambayo inawafanya kuwa na wasiwasi huenda wakakumbana na magonjwa ya mlipuko.
Wananchi wa eneo hilo wameyasema hayo leo Mei 2, ikiwa zimeshapita siku tisa tangu Wizara ya Afya ilipotangaza mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika halmashauri ya jiji la Ilala, huku watu 10 wakithibitika kuwa na ugonjwa huo.
Akizungumza na Mwananchi, Deus Soka amesema licha ya kutangazwa kuwa kuna mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu bado serikali ya kata ya Buza hawajakuwa na muamko wa kuhakikisha maeneo ya mitaa yanakuwa salama.
“Takataka zimekuwa zikirundikwa katika baadhi ya maeneo kwa takribani mwezi mpka miezi jambo ambalo ni chukizo kwa wananchi kwa kuwa zinahatarisha afya zao,” amesema
Ameongeza kwa kusema hata kwa mkandarasi aliopewa tenda ya kuhakikisha takataka zinaondoka ili kuweka mazingira sawa anapaswa kuchukuliwa hatua kwa kuwa ameshindwa kutekeleza kazi yake kwa usahihi.
“Mkandarasi amepewa tenda licha ya wananchi kutoa hela ya kuzoa taka kila mwisho wa wiki bado ameshindwa kutekeleza kazi yake” amesema.
Magreth Dustan ameeleza kwamba wamekua wakipata kero katika mtaa wao hali ambayo wakati wa mvua maji machafu yamekuwa yakitiririka katika maeneo yao ya makazi na kusababisha hatari ya kiafya.
“Kero imezidi kuwa kubwa, mtoto wangu jana alikuwa anasumbuliwa na tumbo leo nimempeleka hospital wameniambia ana dalili za kipindupindu, matatizo haya tukiwaambia viongozi wa mtaa hawatupi majibu yaliyokuwa sahihi” amesema
Naye, Tumsifu Irrma amesema suala la matakataka katika eneo hilo viongozi wanalitambua na wamekua wakikaidi katika kuzitoa huku wakidai mkandarasi ndiye anahusika na jambo hilo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Buza Mohamed Mbagalo amesema changamoto ya hiyo inakwamishwa na mkandarasi kwa kuto kuhakikisha anafanya kazi yake kwa ufasaha kwani walishakaa kikao cha halmashauri ili kutatua changamoto hiyo lakini hakuna kilichofanyika.
“Juzi tulikua kwenye kikao cha kamati ya maendeleo ya kata, kikubwa tulikua tunamlalamikia mkandarasi aliopewa jukumu la kuzoa taka, hivyo moja ya maazimio katika kamati hiyo tuliazimia ni namna gani tutachukua mswada wa kisheria wa kumuondoa mkandarasi” amesema
Ameongeza kwa kusema jambo hilo linawasumbua sana hivyo wameamua kuzipeleka kero hizo katika ngazi ya kata ili ziweze kutatuliwa.
Mwananchi ilipofika katika ofisi za kata, hakukua na Diwani wala Mtendaji wa kata, badala yake alikuepo Afisa Ustawi wa jamii ambaye amekataa kuzungumzia jambo hilo, na kutokutoa majina yake bila ya ushirikiano wowote.