Wakazi wa Tanga waomba huduma za kibingwa kufika hospitali za wilaya, kata
Tanga. Wakazi wa Tanga wameiomba Serikali kuweka utaratibu wa kutoa huduma za madaktari bingwa katika Hospitali za mikoa na wilaya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo jijini Tanga, leo Alhamisi Machi 2 wamesema kupata huduma za kibingwa ni gharama hivyo utaratibu wa kuwafuata wananchi katika hospitali za mikoa zinarahisisha huduma hizo.
Mwanakombo Abdalah mkazi wa Daruni wilayani Mkinga aliyefika Hospitali ya Bombo kupata huduma kutoka kwa madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Kanda ya Rufaa Benjamin Mkapa amesema huduma za afya zimeboreshwa kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo iliwalazimu kusafiri kwenda Muhimbili.
“Katika hili nimpongeze Rais Samia Suluhu Hassan kwa kweli, mimi na wenzangu tumetoka Wilaya ya Mkinga kuja kupata huduma kwa madaktari hawa na nimepata fursa ya kufanya vipimo na sasa nasubiri kwenda kufanyiwa upasuaji hili ni jambo kubwa kwetu sisi wananchi,” amebainisha Mwanakombo.
Naye Mzee Shafii Ally Nuru yeye ameiomba serikali huduma za ujio wa madaktari hao ziwafikie katika Hospitali za wilaya ili kuwanufaisha wananchi wa hali ya chini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Hospitali ya Kanda ya Rufaa Benjamin Mkapa, Dk Henry Humba amesema mpaka leo wameweza kuwaona wagonjwa 400 ambao kati ya hao wagonjwa 19 wamebainika kuwa na matatizo yanayohitaji upasuaji.
Dk Humba amesema katika wagonjwa 400 waliogundulika kuwa na matatizo ya macho ni 194, wanawake wenye matatizo ya uzazi 81, na wenye matatizo ya ubongo na mishipa ya fahamu 5.
“Lengo lilikuwa ni kukutana na wagonjwa 200 kwa siku tano lakini mwitikio umekuwa mkubwa wananchi wenye matatizo mbalimbali wamejitokeza kwa wingi tofauti na matarajio yetu.
“Huduma hizi tunatarajia kumaliza Machi 3, hivyo wagonjwa wengine tumewaona na kuwashauri wengine tumewapatia tiba pia wapo tuliowafanyia upasuaji zipo na kesi zilizohitaji rufaa tumefanya hivyo,” amesema Dk Humba