Wakulima Mnyagala waomba kufutiwa deni la Sh36 milioni

Skimu ya umwagiliaji Mnyagala inayodaiwa kumnufaisha mwekezaji badala ya wakulima wakitoa gunia moja la mpunga kila mmoja wakati wa mavuno na kujisababishia hasara kubwa pasipo wao kutambua. Picha na Mary Clemence
Muktasari:
- Wakulima wanaotumia skimu ya umwagiliaji Mnyagala, wilayani Tanganyika, wameiomba Tume ya Taifa Umwagiliaji (NIRC), kuwafutia deni la Sh36 zitokanazo na ada pamoja na tozo, kwa kuwa hawawezi kumudu malipo hayo.
Katavi. Wakulima wanaotumia skimu ya umwagiliaji Mnyagala, wilayani Tanganyika, wameiomba Tume ya Taifa Umwagiliaji (NIRC), kuwafutia deni la Sh36 zitokanazo na ada pamoja na tozo, kwa kuwa hawawezi kumudu malipo hayo.
Wakizungumza kwa niaba ya wakulima kwenye mkutano wa hadhara leo Augost 23, 2023; viongozi wa skimu hiyo akiwemo Diwani wa Kata ya Mnyagala, Mathias Nyanda, wamesema deni hilo limewashtua baada ya kuwasilishwa kwao na NIRC.
Katibu skimu hiyo, Thomas Thadeo, amesema kabla ya kuweka tozo hizo, viongozi wa mamlaka za juu wanatakiwa kufika na kutembelea mashamba ya wakulima ili gharama ziendane na ukubwa wa shamba.
“Muangalie shida ambazo zipo shambani, matatizo yaliyopo mkilinganisha labda mnaweza kutoa au kupendekeza shilingi ngapi zilipwe badala ya kuambiwa tu lipeni hiki,” amesema Thadeo.
Kwa upande wake Diwani Nyanda amesema ameshtuka baada ya kuelezwa na katibu wa skimu kuwa wanadaiwa Sh36 milioni ambapo kati ya hizo pesa, Sh18 milioni ni deni la jana.
“Nimeshangaa sana wakati tulikubaliana...mlivyosema hapa nimetetemeka, huu utaratibu umeanza lini ujio wenu kumbe mmekuja kutuua kabisa wakulima... tupo chini ya miguu yenu tusaidieni” amesema diwani huyo.
Mhandisi wa NIRC Mkoa wa Katavi, Samson Bai, amesema skimu ya Mnyagala ina changamoto kubwa ya ulipaji ada na tozo za Serikali.
“Msimu uliopita tunadai Sh18 milioni na msimu huu pia wana deni la Sh18 milioni hivyo jumla inakuwa Sh36 milioni, hamjalipa hata senti moja, niombe viongozi simamieni hizi fedha zilipwe,” amesema Bai.
Kwa upande wa Mwanasheria wa tume hiyo, Amina Shimweta, amesema wakulima wamekuwa wakinyonywa na wawekezaji wanaoingia nao makubaliano ya kufanya matengenezo ya skimu bila wao kutambua.
“Mnaibiwa muwekezaji ndani ya mkataba anakwambia amewekeza kwa gharama ya sh40 milioni lakini kwenye mkataba huohuo anakawambia atakusanya Sh200 milioni,” amesema Amina na kuongeza;
“Mkataba una mwanzo hauna mwisho atakusanya hadi mwisho, mwaka huu anatengeza kitu hiki mwaka kesho kingine kila siku mnaibiwa ndiyo maana tunatoa hii elimu.”
Amesema wakulima wanatakiwa kukusanya mazao yao wenyewe na mwekezaji akihitaji kufanya matengenezo, afuate taratibu kwa mujibu wa kifungu cha 20 na 31 cha sheria ya 2021.
“Aje tumpe kibali, atawasilisha michoro na gharama zake, tutafanya tathmini kuona kama gharama hizo ni sahihi...mwekezaji anasema gunia la mpunga ni Sh40, 000 lakini bei ya sokoni ni Sh100, 000...yeye anakusanya faida zaidi,” amesema
Skimu ya umwagiliaji Mnyagala inahudumia zaidi ya wakulima 200 wanaotegemea uchumi wao kupitia kilimo cha mazao tofauti ikiwemo mpunga na mahindi.