Wakulima wa mwani Lindi, Mtwara wanolewa

Fatuma Machalla kutoka mkoani Lindi akiwaelekeza wakulima jinsi ya kuandaa mwani. Picha na Bahati Mwatesa

Muktasari:

  • Wakulima wa zao la mwani wa mikoa ya Lindi na Mtwara walilia kushuka kwa bei huku wakiomba wanunuzi kujitokeza ambapo kwa sasa wanauza  kwa Sh500 kutoka bei ya awali ya Sh1000.

Lindi/Mtwara. Kutokana na kukosekana kwa soko la mwani ghafi katika mikoa ya Lindi na Mtwara, Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa mafunzo kwa washiriki 120 kuhusu namna kuongeza thamani ya zao hilo.

Akizungumza katika mafunzo hayo leo Aprili 21, 2024, Ofisa uvuvi kutoka wizara hiyo, Happiness Kapinga amesema mafunzo hayo yataimarisha soko la mwani baada ya kuongezewa thamani.

Amesema kukosekana kwa soko la mwani ghafi kumeleta changamoto kubwa kwa wakulima, hivyo kuongezwa thamani kunaweza kuongeza mauzo ya bidhaa hizo.

“Katika kukabiliana na changamoto ya soko, Serikali imeanza kutoa elimu ya uchakataji wa zao hilo ili wakulima wazalishe bidhaa zao, kwa mwani uliosindikwa badala ya kuuza ukiwa ghafi,”amesema.

Pamoja na hayo, amesema mwani una faida nyingi ambapo  madini yake yanasaidia  kuboresha mifumo ya binadamu ambayo haifanyi kazi vizuri ikiwemo mzunguko wa damu, huimarisha ukuaji bora wa akili kwa watoto wadogo, na ni lishe bora kwa mama mjamzito na anayenyonyesha.

Kwa upande wake, mkulima wa zao hilo kutoka halmashauri ya Mtama mkoani Lindi, Fatuma Ayubu amesema kutokana na mvua kubwa zinazonyesha kusababisha kukosa wanunuzi wa mwani, wameyumbishwa kiuchumi na kupata hasara.

“Yaani hakuna wanunuzi mwani unaharibika, tunapata hasara, soko hakuna na ukiangalia sisi wengine tunategemea zao hili kuendesha familia zetu. Kukosekana kwa wanunuzi kunatupa wakati mgumu zaidi,” amesema Fatuma.

Mariamu Shaibu, mkulima wa mwani kutoka wilaya ya Kilwa amesema changamoto kubwa iliyopo sasa ni kupunguza uzalishaji kutokana na mvua nyingi ambazo zinasababisha bahari kujaa maji na kuathiri uzalishaji.

Naye Zuhura Chimpele, mkulima wa mwani kutoka katika kijiji cha Mkungu, amesema bei ya mwani imekuwa changamoto kubwa ambapo awali waliuza bidhaa hiyo kwa Sh1,000 ikashuka hadi Sh700 na sasa Sh500.