Wakulima walia na uharibifu wa wanyama shambani

Mkazi wa Kijiji cha Sanya wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, Christna Simon mkulima katika Mashamba ya Leon akionyesha mahindi yaliyoharibiwa na tembo

Muktasari:

  • Wakulima wilayani Siha Mkoa wa Kilimanjaro wameomba maofisa maliasili kuwasaidia kuwafukuza wanyama wanaotoka hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) na kuharibu mazao yao shambani.

Siha. Wakulima wa mashamba ya Leoni na Pongo wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro wameomba maofisa maliasili kuwasaidia kuwafukuza wanyama wanaotoka hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) na kuharibu mazao yao shambani.

Wakizungumza na waandishi wa habari leo Jumai Mosi, wakulima hao wamesema pamoja na kuhudumia mashamba yao kwa gharama kubwa, hawana uhakika wa mavuno.

"Wanaume wanalala mashambani na tembo wakija wanapiga kelele kwa kutumia madebe, kuwasha moto na kuwasha tochi, lakini ulinzi huu sio salama kwao, hivyo tunaomba maafisa maliasili wao ndiyo wamesomea kazi hii watusaidie," amesema Christina Simon.

Simon mwenye shamba la ukubwa wa ekari mbili, anasema limeharibiwa na wanyama.

Kwa upande wake Oscar Mmari amesema amekodi shamba kwa Sh100, 000 kutunza mazao aliyopanda kwa gharama ya Sh500,000 lakini tembo wameharibu mazao yote

“Tunaomba Serikali iingilie kati suala hili, kwani ni kwa miaka mitatu mfululizo hatukupata mazao ya uhakika kutokana na mvua kunyesha chini ya kiwango na mwaka huu mvua ni nyingi mazao mazuri, lakini tembo wanaleta usumbufu.

"Watusaidie sio wasubiri wanyama waharibu mazao halafu waje watulipe kifuta jasho Sh40,000 au Sh50,000 kwa ekari moja wakati tumetumia gharama kubwa," amesema Mmari

Akizungumzia malalamiko ya wakulima hao, Ofisa Maliasili wilayani humo, Onesmo Haule amesema wamefika eneo la mashamba hayo na wataendelea kuhakikisha mazao ya wananchi yanakuwa salama.

Naye Mwenyekiti wa CCM wilayani humo, Wilfred Mosi amesema Julai 2 atafika kuwatembelea na kuangalia jinsi ya kuwasaidia.