Wakulima watakiwa kutumia mbolea za mimea

Muktasari:
Wakulima wa mazao ya mpunga na mahindi wilayani Geita wameshauriwa kutumia mbolea yenye virutubisho vya mimea inayoboresha mazingira ya mmea na kuufanya udongo kuwa na rutuba ili walime kilimo chenye tija na kujikwamua kiuchumi.
Geita. Wakulima wa mazao ya mpunga na mahindi wilayani Geita wameshauriwa kutumia mbolea yenye virutubisho vya mimea inayoboresha mazingira ya mmea na kuufanya udongo kuwa na rutuba ili walime kilimo chenye tija na kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza kwenye maonyesho ya nne ya Fahari ya Geita yanayoendelea kwenye viwanja vya Kalangalala mjini Geita,Meneja Mauzo na Masoko kutoka Kampuni ya Itracom Fertilizers LTD inayotengeneza mbolea ya Fomi Amos Projest amesema matumizi sahihi ya mbolea yatawezesha wakulima kuvuna mazao mengi na kujipatia kipato.
Amesema mbolea zinazozalishwa na kampuni hiyo ni za mseto wa mbolea za asili ikiwemo samadi na mbolea za chumvi chumvi hali itakayopelekea ardhi kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kuzalisha mazao kwa wingi.
“Tumejikita sana na uboreshaji wa afya ya udongo kwa kulinda viumbe hai wanaoishi ardhini kwa kuwa ardhi ina uhai, hivyo kwa kufanya hivyo itamsaidia mkulima kuvuna mazao kwa wingi na kumwinua mkulima kutoka kilimo cha mazoea hadi kilimo chenye tija,”amesema Projest
“Watu wamezoa kutumia mbolea za viwandani au za asili peke yake sisi kwa kutambua watu wanataka waongeze mavuno au wazalishe kwa zaidi lakini wakati huo huo wanatakiwa walinde afya za udongo lazima kuwe na uasili kwenye mbolea zinazozalishwa ndio maana tukaamua kuja na teknolojia ya mbolea iliyotafitiwa, inaubora na imethibitishwa na mamlaka za ubora”amesema Projest
Projest amewataka wakulima kuondoa dhana ya kuwa watavuna bila kutumia mbolea lakini pia akawataka watumie mbolea inayolinda afya ya udongo itakayomuwezesha kuzalisha zaidi na kuacha udongo ukiwa salama.
“Wakulima waliweka matumizi ya mbolea pembeni wakiamini ardhi ni nzima haina tatizo lakini wanatakiwa kujua wanapovuna kunavirutubisho vinaondoka ardhini na vinatakiwa viongezwe kwa njia ya mbolea na hata wanaotumia mbolea wanashindwa kutumia matumizi sahihi na mwisho wa siku wanajikuta wakipata hasara elimu ya matumizi sahihi ya mbolea ni muhimu kwa mkulima”amesema Projest
Mkulima wa Mpunga wilayani Geita, Ester Joseph amesema kupitia matumizi ya mbolea amefanikiwa kuvuna mazao mengi ikilinganishwa na miaka ya nyuma aliyokuwa akilima bila kuweka mbolea shambani.
Mkurugenzi wa kampuni ya Afrikan Creative ambaye ni Mwenyekiti wa maonyesho hayo yaliyoanza Mei 26, 2023 amesema maonyesho hayo yenye kauli mbiu ya Kilimo, ufugaji na uvuvi ni nguzo ya maendeleo yanayowawezesha wananchi kupata elimu kutoka kwa wadau mbalimbali.
Amesema mbali na Wajasiriamali kufanya biashara lakini elimu ya kilimo cha kisasa inayotolewa na makampuni yanayojishughulisha na kilimo kwenye eneo hilo itawezesha wakulima kuondoka kwenye kilimo cha mazoea na kulima kwa tija ili kujikwamua kiuchumi.