Walalamikia kutozwa faini ya Sh1 milioni kwa ugomvi wa kifamilia

Mbunge wa Kishapu, Boniface Butondo akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika Kijiji cha Nhobola Wilaya ya Kishapu. Picha na Suzy Butondo

Muktasari:

Wakazi wa Kijiji cha Nhobola Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamelalamikia faini ya kati ya Sh300, 000 hadi Sh1 milioni wanayotozwa na walinzi wa Jeshi la Jadi maarufu kama Sungusungu kwa makosa ya kijamii ikiwemo ugomvi wa kifamilia.

Shinyanga. Wakazi wa Kijiji cha Nhobola Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamelalamikia faini ya kati ya Sh300, 000 hadi Sh1 milioni wanayotozwa na walinzi wa Jeshi la Jadi maarufu kama Sungusungu kwa makosa ya kijamii ikiwemo ugomvi wa kifamilia.

Akizungumza wakati wa mkutano wa mbunge wa Kishapu, Boniface Butondo uliolenga kusikiliza na kutatua kero za wananchi uliofanyika kijijini hap oleo Oktoba 5, 2023, mkazi wa kijiji hicho, Juliana Bilu amesema wanaoshindwa kulipa faini hiyo huadhibiwa kwa kutengwa katika shughuli mbalimbali za kijamii.

‘’Vitendo hivyo vina harufu ya rushwa kwa sababu wakati mwingine wahusika hutumia madai ya kutunga kuhalalisha faini. Tumechoka na tunaiomba Serikali kushughulikia na kukomesha vitendo hivyo,’’ amesema Juliana

Hoja hiyo imeungwa mkono na Lupande Salala akimwomba mbunge Butondo kutumia nafasi na ushawishi wake kuzuia uonevu unaofanyika kwa wananchi.

"Tatizo lingine tunaloiomba Serikali ishughulikie ni kutosomwa kwa mapato na matumizi ya fedha za umma zinazokusanywa kijijini hapo kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo faini hizo,” amesema Salala

Ukatili na unyanyasaji kijinsia dhidi ya wanawake, watoto na wote wanaotuhumiwa kwa makosa mbalimbali kijijini hapo ni miongoni mwa tuhuma zilizorushwa dhidi ya sungusungu wa kijiji hicho.

Diwani wa Kata ya Talaga kilipo kijiji hicho, Richard Dominick amekiri kuwepo kwa madai mbalimbali dhidi ya sungusungu katia vijiji vya kata hiyo huku akifichua kwamba tuhuma nyingi zinazosababishwa faini huibuliwa, kupigiwa kura na kuidhinishwa na wananchi wenyewe.

"Tumeshawaagiza wenyeviti wa vijiji kuitisha vikao kutathmini kazi za sungusungu katika maeneo yao na kuchukua hatua kukomesha yote yanayolalamikiwa na wananchi,’’ amesema diwani Dominick

Mwenyekiti wa Kijiji cha Nhobola, Kangala Lubarigi amesema kutokana na malalamiko hayo, uongozi wa Serikali ya kijiji itavunja na kuunda upya kamati ya sungusungu, kufanya uchaguzi na kuchukua hatua dhidi ya wanaotuhumiwa kukiuka taratibu.

Kutokana na taarifa hizo, Butondo ameahidi kuwasilisha malalamiko ya wananchi kwenye mamlaka husika kwa ufumbuzi huku akimwagiza diwani kupitia vikao halali kushughulikia na kumaliza malalamiko ya wananchi yaliyoko ndani ya uwezo na mamlaka yao.

"Diwani simamia utatuzi ya matatizo ya wananchi katika eneo lako, hili la wananchi kulalamikia faini na vitendo vinavyokiuka sheria litashughulikiwa na mamlaka za Serikali ikiwemo ofisi ya Kamanda wa Polisi Wilaya (OCD) Wilaya ya Kishapu," amesema mbunge Butondo