Walichosema watoto wakiadhimisha siku yao Afrika

Muktasari:
- Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa jamii na wazazi kuona jukumu la ulinzi wa watoto linawahusu wote. Ametoa kauli hiyo Siku ya Mtoto wa Afrika inayoadhimishwa kila Juni 16 ya mwaka na nchini humo imeadhimishwa maeneo mbalimbali.
Dar/mikoani. Usiri wa jamii unapofanyika ukatili kwa watoto, ni moja kati ya sababu iliyotajwa na watoto wenyewe kuwa inachangia kuendelea kuwapo kwa vitendo hivyo dhidi yao.
Kwa mujibu wa watoto hao, pamoja na kundi hilo kuwa katika hatari ya kukatiliwa, aghalabu jamii imekuwa ikiwaficha wanaotenda vitendo hivyo, jambo linalowafanya waendelee kukumbwa na vitendo hivyo.
Sambamba na mtazamo huo wa watoto, Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza umuhimu wa jamii na wazazi kuona jukumu la ulinzi wa watoto linawahusu wote.
Watoto hao walitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti, katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, inayoadhimishwa Juni 16, kila mwaka na kwa Tanzania iliadhimishwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu 'Elimu jumuishi kwa watoto izingatie maarifa, maadili na stadi za kazi.’
Hoja za watoto
Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Watoto Wilaya ya Kinondoni, Gift Mussa amesema usiri wa jamii dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto ndio unaosababisha kundi hilo liendelee kukatiliwa.
Mussa amesema mara nyingi usiri huo hufanyika pale ambapo jamii itagundua mtoto amefanyiwa ukatili, hali aliyodai inawarudisha nyuma katika kila jambo, ikiwemo masomoni.
"Tuna changamoto nyingi, lakini ya ukatili inatuathiri na inaturudisha nyuma katika maendeleo ya darasani," amesema.
Ukatili dhidi ya watoto ni miongoni mwa sababu za ongezeko la watoto wa mitaani, kama inavyoelezwa na mtoto Maria Moses anayesoma kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Mafiga, mkoani Morogoro.
Ameeleza watoto huamua kukimbilia mitaani baada ya kubakwa na wakati mwingine kulawitiwa.
Mkoani Arusha nako watoto wanalalamikia kuingizwa katika ndoa za utotoni na hivyo kuathirika kama ilivyosimuliwa na Felister Nicolaus (14) kupitia risala aliyoisoma katika maadhimisho hayo, mkoani humo.
Kwa mujibu wa mtoto huyo, watoto wengi nchini wameendelea kuwa waathirika wa vitendo vya ukatili kwa kutelekezwa.
“Tunaingizwa kwenye ndoa za utotoni, mambo yote haya yanaathiri malezi na makuzi yetu, kimwili na kifikra na yanakatisha ndoto zetu za maisha,” amesema Felister.
Rais Samia
Rais Samia aliadhimisha siku hiyo Ikulu, Dar es Salaam, akiwa na watoto mbalimbali, huku akisisitiza jamii kushirikiana katika malezi bora yatakayosababisha maadili mema kwa watoto.
Ametaka hilo liambatane na kuhakikisha usalama wa kila mtoto unakuwa jukumu la jamii kwa ujumla.
Uzalendo katika umri mdogo na elimu ni mambo mengine yaliyohimizwa na Rais Samia, alipozungumza katika maadhimisho hayo.
Akizungumzia kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema urithi wa elimu ni bora zaidi kuliko urithi mali, kwa kuwa mtoto hatafilisika.
"Unapompa mtoto urithi wa elimu unakuwa umewekeza jambo kubwa kwenye maisha yake na hata akiwa mkubwa ataitumia elimu hiyo kwa manufaa yake na jamii inayomzunguka," amesema.
Kauli za wakuu wa wilaya
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amesema kuna kazi ya kufanya kuhakikisha watoto wanatatuliwa changamoto zao.
"Wana Kinondoni tunatakiwa kuwalinda na kuwatetea watoto katika maeneo yetu, kwani Rais Samia Suluhu Hassan amebeba ajenda ya kumlinda mtoto kwa hali na mali hivyo tunapaswa kumlinda mtoto kwa kutoa taarifa,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengewa amesema sababu kubwa ya mmonyoko wa maadili ni kukua kwa teknolojia na baadhi ya wazazi kupwaya kwenye malezi.
“Marufuku baadhi ya shule na walimu kupokea misaada ya vitabu au vitendea kazi vyovyote bila kupata idhini ya ofisi yangu, baadhi vimekuwa vikihamasisha vitendo vya mmomonyoko wa maadili,” amesema Mtahengewa.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, Sara Ndaba amesema changamoto kwa sasa ni jinsi ya kuwaepusha watoto hasa wa mitaani dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Naye, Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema wazazi kuwaacha watoto kwenda vibanda umiza yamekuwa chanzo cha matukio ya ukatili ambapo watoto wamekuwa wakilawitiana.
“Wazazi na walezi wakiwajibika kufundisha maadili mema yatasaidia kupunguza ama kumaliza matukio ya ukatili katika mkoa huu kumuacha mtoto kujilea mwenyewe kama bata anavyolea watoto wake hiyo ni hatari,” amesema Mkama.
Mkurugenzi Mkaazi wa Shirika la SOS Children's Village Tanzania, Florian Fanuel amesema changamoto zinazowakabili watoto hazijabadilika, shina la tatizo likaanzia kwenye malezi ya watoto ndani ya familia.
"Kuna watoto wengi wazazi wao wapo wote wawili, lakini hao wazazi hawapati nafasi ya kuwalea watoto wao vizuri, hivyo watoto hutoroka nyumbani. Kuna familia baba au mama analea mtoto mwenyewe mazingira hayo yanatengeneza matatizo katika utoaji wa huduma bora,” amesema.
Imeandikwa na Devotha Kihwelo,Baraka Loshilaa(Dar),Bertha Ismail(Arusha), Juma Mtanda, Johnson James(Morogoro),Joseph Lyimo (Manyara)