Walimu kizimbani tuhuma za udanganyifu wa mtihani

Muktasari:

Walimu watano wa shule ya msingi Siashimbwe wamefikishwa mahakamani mjini Moshi  wakituhumiwa kufanya udanganyifu katika mtihani wa taifa wa darasa la saba uliofanyika Oktoba, 2020.


Moshi. Walimu watano wa shule ya msingi Siashimbwe wamefikishwa mahakamani mjini Moshi  wakituhumiwa kufanya udanganyifu katika mtihani wa taifa wa darasa la saba uliofanyika Oktoba, 2020.

Watuhumiwa hao waliosomewa mashitaka yao leo Novemba 27, 2020 mbele ya hakimu mkazi wa Moshi, Naomi Mwerinde wakidaiwa  kutenda makosa manne ya udanganyifu.

Akiwasomea mashtaka hayo wakili wa Serikali kutoka ofisi ya taifa ya mashtaka, Nitike Emmanuel ametaja makosa hayo manne ni pamoja na kutoa mitihani ya Hisabati na Kiswahili kutoka nje ya chumba cha mitihani.

Amesema  mnamo Oktoba 7, 2020 katika maeneo ya shule hiyo watuhumiwa walitoa karatasi ya mtihani wa hesabu kutoka chumba cha mtihani kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Amesema kosa la pili washtakiwa hao walishindwa kutunza karatasi ya mtihani wa Kiswahili kwa kutoa karatasi hiyo ndani ya chumba cha mtihani.

Nitike ametaja  kosa la tatu linalomkabili mshtakiwa wa kwanza kuwa alikutwa na karatasi ya majibu ya mtihani wa Kiswahili wa darasa la saba na kosa la nne kwa mshtakiwa huyo ni kukutwa akiwa na majibu ya mtihani wa hesabu  wa darasa la saba

Washitakiwa hao wanaotuhumiwa kufanya udanganyifu katika mtihani wa darasa la saba ni Philip Kalengi, Fredrick Lyaruu, Flora Maambo, Elionora Shirima pamoja na Elistika Tesha ambapo baada ya kusomewa mashitaka yao wamekana mashtaka.

Washtakiwa hao walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na kurudishwa rumande huku kesi hiyo ikiahirishwa hadi Desemba 11, 2020.