Walimu Kondoa walalamikia wanasiasa

Mkuu wa idara ya Elimu na mafunzo wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Stella Kiyoba

Muktasari:

  • Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kimewanyooshea kidole wanasiasa kwamba wanaingilia majukumu yao hata mahali ambapo hawastahili.


Kondoa. Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kimewanyooshea kidole wanasiasa kwamba wanaingilia majukumu yao hata mahali ambapo hawastahili.

Kauli hiyo imetolewa Oktoba 5, 2022 na Mwenyekiti wa CWT wilaya ya Dodoma, Prosper Mutungi kwenye mdahalo wa kilele cha siku ya Mwalimu duniani ambayo kimkoa imefanyika Kondoa.

Mutungi amesema kuna baadhi ya maeneo madiwani huingia kukagua hadi maandalio ya masomo kwa walimu licha ya kuwa wao ni si wataalamu.

"Unakuta mtu ni diwani wa kata halafu anafika ofisini kwa walimu halafu anafanya ukaguzi, hivi jiulize huyu anakagua kitu gani sasa," amesema Mutungi.

Katika hatua nyingine CWT kimetaja mambo manne kuwa kikwazo kwa walimu katika kutimiza malengo yao na kupelekea msongo wa mawazo hata washindwe kufundisha ipasavyo.

Mambo hayo ni uhaba wa nyumba za kuishi, mishahara, kutokuwepo mafunzo kazini na posho ya kufundishia lakini suala la kupewa vinyago kwa shule inapofanya vibaya inawagawa pia.

Mkuu wa Idara ya Elimu na Mafunzo wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT), Stella Kiyabo alisema mwalimu ni kitovu cha elimu lakini inashangaza mambo mengi yanafanywa na Serikali lakini walimu wanasahaulika.

Kiyabo ameseema ili kuwepo na elimu bora, inapaswa vichwa vya walimu vijengewe maarifa lakini akasema inashangaza kuwa Serikali imeweka mkazo kuboresha elimu kabla ya kuboresha vichwa vya walimu.

Naye Deus Bwahama alisema pamoja na kilio walichonacho walimu lakini maeneo mengi nao wamejisahau na sasa wanakiuka maadili ya utumishi ikiwemo mavazi ambayo yanatoa picha mbaya kwa wanafunzi.