Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Walioathiriwa mafuriko maji ya Bwawa la Nyerere wasaidiwa

Mwonekano wa mojawapo ya maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo wilayani Rufiji

Muktasari:

Fedha hizo ametoa kusaidia ununuzi wa mbegu kwa zaidi ya wakazi 1,000 wilayani Rufiji ambao mali, mashamba na makazi yao yameathiriwa na mafuriko.

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa, ametoa Sh40 milioni kusaidia ununuzi wa mbegu kwa zaidi ya wakazi 1,000 wilayani Rufiji ambao mali, mashamba na makazi yao yameathiriwa na mafuriko.

Mafuriko yalitokana na maji yaliyofunguliwa kutoka bwawa la uzalishaji umeme la Julius Nyerere (JNHPP).

Tathimini ya awali imebaini nyumba 58 zimeharibika na wakazi 951 wameondolewa katika maeneo yao, huku zaidi ya hekta 28,374.74 za mazao ya kilimo na biashara yakiwamo mahindi, mpunga, ufuta na migomba zimeathiriwa na mafuriko.

Mchengerwa ambaye ni mbunge wa Rufiji, mkoani Pwani amefanya ziara kukagua athari ya mafuriko hayo na kutoa fedha hizo leo Aprili 3, 2024 akieleza amelenga kuwatia moyo waathirika na kuwawezesha kurejea kulima upya baada ya mazao yao kusombwa na mafuriko.

“Hili ni janga letu sote mimi na ninyi, tuliamini kwamba ujenzi wa JNHPP utakuwa mkombozi wa mafuriko ambayo yamekuwa yanatukumba mara kwa mara lakini kwa bahati mbaya bado hali hii imejitokeza," amesema.

"Tuendelee kuwa na imani kwamba mradi ukikamilika huenda changamoto hii ikawa imetatuliwa,” amesema.

Waziri Mchengerwa amesema, “Ninafahamu namna wakazi wa Rufiji mlivyokuwa mmelima kweli-kweli mwaka huu. Ninaomba turejee shambani tulime tena kwa kiwango kikubwa. Ninamkabidhi mkuu wa wilaya Sh40 milioni kwa kuanzia kwa ajili ya kusaidia ununuzi wa mbegu ili turejee shambani tupande tena tusije kufa kwa njaa.”

Amesema fedha hizo alidunduliza kutoka kwenye mshahara wake kwa ajili ya kuandaa futari ya pamoja katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kama anavyofanya kila mwaka.

"Kwa hali hii ya mafuriko niseme tu kwamba futari si kitu, nalazimika kuitoa kwa ajili ya ununuzi wa mbegu, nitaenda kuwaomba marafiki zangu wanichangie angalau tufikishe Sh100 milioni kwa ajili ya kuwasaidia wana-Rufiji walioathirika na mafuriko haya,” amesema.

Ametoa wito kwa taasisi na mashirika ya misaada ya kibinadamu, na wasamaria wema kuguswa kuwashika mkono kwa namna moja au nyingine wananchi hao kipindi hiki ambacho Serikali ya wilaya inaendelea na ufuatiliaji na tathimini ya athari za mafuriko hayo kwa ujumla.

Halima Mbwana, mkazi wa Kijiji cha Chumbi, ambaye ni miongoni mwa waathirika wa mafuriko hayo amedai hali inazidi kuwa mbaya kuanzia kupata chakula, malazi na makazi.

“Tumesalia watupu, mazao shambani yamesombwa na maji na hata vyakula vya ziada tulivyokuwanavyo vimesombwa pia, nyumba nazo zimesombwa na maji sasa hatuna pa kuishi wala hatuna chakula. Tunaomba tusaidiwe maana hali zetu ni mbaya,” amesema Mbwana.

Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele amesema tathimini ya awali imebaini nyumba 58 zimeharibika, na jumla ya wakazi 951 waliokuwa wakiishi kwenye vitongoji vya Kanga, Kiegele, Kilindi na Nyandote katika Kata ya Chumbi wameondolewa katika maeneo yao nakuhamishiwa sehemu salama.

Amesema zaidi ya hekta 28,374.74 za mazao ya kilimo na biashara yakiwamo mahindi, mpunga, ufuta na migomba vimeathiriwa na mafuriko.