Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waliofariki kwa ajali iliyotokea Same, wazikwa

Muktasari:

  • Miili hiyo ya Irene Salehe, Erine Ndarai na Anjela Mshana imeagwa leo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Pare, Same mjini na kuzikwa katika makaburi yaliyopo karibu na kanisa hilo.

Moshi. Mamia ya wananchi wilayani Same mkoani Kilimanjaro, wamejitokeza kushiriki maziko ya watu watatu wa familia tatu tofauti waliofariki dunia katika ajali ya magari mawili ya abiria yaliyogongana na kuwaka moto wilayani humo.

Miili hiyo ya Irene Salehe, Erine Ndarai na Anjela Mshana imeagwa leo Ijumaa Julai 4, 2025 katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Pare, Same mjini na kuzikwa katika makaburi yaliyopo jirani na kanisa hilo.

Jana, miili ya watu 36 kati ya 42 iliyoteketea kwa moto katika ajali hiyo, iliagwa kimkoa katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya utaratibu wa maziko, ambao baadhi yao walizikwa jana na wengine leo.

Ajali hiyo ilitokea Juni 28, 2025 katika eneo la Sabasaba, Same mjini ikihusisha basi Kampuni ya Chanel One lililokuwa likitokea Moshi kwenda Tanga na basi dogo aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Same Mjini kwenda Moshi kugongana uso kwa uso na kuwaka moto wakati abiria wakiwa ndani ya magari hayo.

Waliofariki dunia katika ajali hiyo ni watu 42 na  31 waliokuwa kwenye Coaster waliokuwa wakienda harusini mjini Moshi, huku kwenye basi la Chanel One wakifariki watu 11.

Akihuburi katika ibada ya mazishi ya watu hao, Mchungaji Selevanus Mshana wa kanisa hilo, amesema tukio hilo la kutisha na lililokatisha uhai wa ndugu zao halikutazamiwa, hivyo amewaomba wananchi kuendelea kuwa na moyo mkuu katika kipindi hiki kigumu.

Amesema ni kipindi ambacho familia zinapaswa kukaa pamoja na kuonyesha upendo wa hali na mali.

"Mungu awabariki sana lakini niwashukuru watu wote ambao kweli mmeshiriki pamoja nasi, hili ni tukio ambalo hakuna mwanadamu ambaye alilitazamia, niwashukuru sana wananachi wa Same, faraja ya Mungu ikae pamoja nasi," amesema mchungaji huyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi la mbele la upande wa kulia la basi la Chanel One na dereva kukosa mwelekeo akashindwa kulimudu gari na kuhama upande wa kulia wa barabara alikogongana uso kwa na Coaster kabla ya kuwaka moto.