Advertisement

Waliojiunganishia umeme kinyume cha sheria wahukumiwa kulipa fidia ya Sh 15.8m

Saturday November 21 2020
tanesco pic
By Hadija Jumanne

 Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu, wafanyabiashara watatu kulipa fidia ya Sh 15.8milioni baada ya kupatikana na hatia ya kuisababishia hasara Shirika la Umeme nchini (Tanesco)

Washtakiwa hao ni  Gaston Masika(58), Gerald Mmasi(58)mkazi wa Mvomero mkoani Morogoro na Freeman Shirima(48)mkazi wa Mbezi juu, ambao wote walikuwa wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 68/2020.

Mbali na adhabu hiyo, Mahakama hiyo imewahukumu kila mmoja kulipa faini ya Sh 200,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita jela, endapo watashindwa kulipa faini hiyo.

Hata hivyo, washtakiwa hao wamefanikiwa kulipa fidia na faini na hivyo kukwepa kifungo.

Hukumu hiyo imetolewa leo, Novemba 20,2020 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Kassian Matembelea, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa hoja za awali.

Hakimu Matalembele amesema  washtakiwa wametiwa hatiani kwa kosa la kuingilia miundombinu ya Tanesco na  kuisababishia hasara Tanesco ya Sh 15.8milioni.

Advertisement

Washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka matatu lakini, wametiwa hatiani katika shtaka moja la kuingilia miundombinu ya Tanesco na kuiba umeme, baada ya kukiri mashtaka yao na kufikia makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP).

" Mahakama imewatia hatiani katika shtaka moja kama mlivyoshtakiwa, hivyo mnatakiwa kulipa fidia ya Sh 15.8milioni kwa pamoja, “ amesema Hakimu Matembele.

Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo,  wakili wa Serikali Mkuu, Materus Marandu amedai kuwa shauri hilo liliitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali na kisha kusomewa hati ya mashtaka, baada ya kufanya makubaliano na DPP ya kuimaliza kesi  hiyo.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa Februari 2, 2016 katika eneo la Mwenge, barabara ya Sam Nujoma, wilaya ya Kinondoni,  kwa makusudi na ukiukwaji wa sheria, waliingilia miundombinu iliyowekwa kwa ajili ya kusambaza huduma za umeme hivyo kuisababishia hasara ya Tanesco.

Advertisement