Waliomfuata Kambaya Chadema nao wajitoa

Tukio la Abdul Kambaya akitangaza kujiondoa uanachama wa Chadema.
Muktasari:
- Waliokuwa wakidaiwa kuwa wanachama wa CUF waliojiunga na Chadema wiki mbili zilizopita wametangaza kujitoa wakidai kutopewa ushirikiano kwenye chama hicho.
Dar es Salaam. Siku mbili baada ya Abdul Kambaya na wenzake tisa kuondoka Chadema, kundi lingine la watu zaidi ya 600 lililojiunga na chama hicho kutokea CUF hivi karibuni limefuata nyayo hizo.
Pamoja na sababu iliyotajwa na Kambaya kwamba kuondoka kwake kumetokana na kutotimiziwa kile alichoahidiwa, wakizungumza na vyombo vya habari, wanachama hao wametaja na nyingine kuwa kukosa ushirikiano kutoka kwa viongozi wa ngazi ya chini ya Chadema.
Hata hivyo, mmoja wa wanachama hao, Shahada Issa aliwaambia waandishi wa habari juzi jana, hakukuwa na makubaliano ya ahadi yoyote wakati wanajiunga na chama hicho.
“Kwenye mchakato wa kujiunga na Chadema hatukuwa na makubaliano yoyote badala yake tulizungumza kwamba tunaingia kwenye chama ili kufanya kazi,” alisema Issa.
Kuna dalili kwamba uamuzi wa wanachama hao zaidi ya 600 ulifahamika mapema na Kambaya, kwa kile alichokitabiri juzi alipoulizwa na gazeti hili akisema: “Tujipe muda kesho (jana) linaweza kutokea lolote”.
Idadi hiyo ya walioondoka, inafanya waliojiunga Chadema hivi karibuni kutokea CUF wasalie wawili, badala ya 604 wa awali.
Akitangaza uamuzi huo kwa niaba ya wenzake jijini Dar es Salaam leo Mei 6, Abdallah Mng’ae amesema ukiukwaji wa makubaliano na kutopewa ushirikiano na viongozi wa ngazi ya chini ni sababu mojawapo ya kujiondoa kwao.
Mng’ae alisema katika kundi hilo anaondoka na wanachama wanaodaiwa kuwa 200 waliojiunga na Chadema hivi karibuni.
“Mimi na wenzangu kama tulivyoamua kuingia katika chama hiki, tumeamua leo kutangaza kujitoa Chadema, maana yake zile nafasi ulizokuwa nazo zinaondoka moja kwa moja,” amesema.
Mng’ae aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chadema Kata ya Mnyamani siku moja baada ya kujiunga na chama hicho, ametaja changamoto aliyokutana nayo wakati anagombea nafasi hiyo.
“Nilipokwenda kuchukua fomu nikaambiwa wanachama wanapoingia wanatakiwa wakajifunze, alafu wakae kwa muda, kisha ndiyo waje kugombea baada ya muda kupita.
“Kwa mimi ninayejitambua nilitumia nafasi yangu kutafuta haki yangu ya msingi ndiyo nikapata nafasi ya Uenyekiti, lakini kuna watu wanaweza kuzikosa kwa kuwa inahitaji umahiri kuyaendea hayo,” amesema.
Kwa mujibu wa Mng’ae, yanayozungumzwa na Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe kwamba kila mwanachama ana haki sawa kama mwingine hayatekelezwi katika ngazi ya chini.
Mwanachama mwingine, aliyetangaza uamuzi huo akiwa na wenzake wanaodaiwa kuwa 401, Said Mwinyi alirejea sababu zilizotajwa na kundi lililoongozwa na Mng’ae.
Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kinondoni, Henry Kilewo hakueleza chochote kwa kile alichofafanua kuwa yupo nje ya Dar es Salaam na hana taarifa hizo.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, Kambaya amesema uamuzi wa wanachama hao kuondoka haukutokana na shinikizo lake, bali ni hasira ya kile kilichozungumzwa na wenzao kwenye mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Chadema.
“Jana nilitabiri kwamba lolote linaweza kutokea kwa kuwa nilijua kuwa kauli zile zilizozungumzwa zitawapa hasira hawa waliokuwa nao kwa hiyo nilijua chochote kitatokea,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu ubunge wa Kinondoni, alisema kulihitajika maandalizi ya mgombea mapema akifananisha na uyoga kwamba: “Wagombea hawaibuki siku hiyo hiyo bali huandaliwa hata uyoga unaanza taratibu unachomoza ndipo unaanza kukua, huwezi kusema ni mapema mno hii ni 2023 unasemaje ni mapema mno.”