Waliorejeshwa shule kupewa elimu afya ya akili

Mkurugenzi wa Save Heaven Foundation, Dk Khadijah Hassan (kushoto), akizungumza na wanafunzi wa Sekondari Tuliani iliyopo Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam.
Muktasari:
- Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, imesema jumla ya wasichana 150 waliokuwa wamekatisha masomo yao baada ya kupata changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito, wamerejea masomoni.
Dar es Salaam. Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam, imesema jumla ya wasichana 150 waliokuwa wamekatisha masomo yao baada ya kupata changamoto mbalimbali ikiwemo ujauzito, wamerejea masomoni.
Hayo yamebainishwa leo Julai 19, 2023 na Ofisa Elimu Maalum wa halmashauri hiyo Laititi Mwombeki, hayo wakati wa ugawaji wa taulo za kike katika shule ya Sekondari Tuliani iliyopo Wilaya ya Kinondoni ambayo ni kituo pia cha wanafunzi waliorejea tena shule.
Mwombeki amesema tofauti ya wanafunzi hao 150 na wale walio katika mfumo rasmi, ni kuwa: “Hawa waliorejea wanajitambua na wanafahamu nini ambacho kimewarudisha shuleni sio wa kuwafutilia sana bali hujituma wenyewe.”
Ikumbukwe Novemba 2021 chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali ilitangaza kuruhusu wanafunzi kurudi shule, hatua ambayo iliondoa agizo la mwaka 2017, lililokataza wanafunzi waliopata ujauzito kuendelea masomo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Safe Haven Foundation, Dk Khadijah Hassan, amesema pamoja na mambo mengine, taasisi yake inatarajia kuanza kutoa elimu ya afya ya akili kwa wanafunzi hao.
Dk Khadija amesema watoto hao pamoja na mambo mengine pia wanakabiliwa na msongo wa mawazo hivyo wameona kuna haja ya kupawa pia elimu ya afya ya akili ili wamalize masomo yao salama.
“Tumekuwa tukishughulika na wanafunzi waliopo shuleni, lakini kwa kuwa na hawa waliorejea shule wameshaathirika, hatuwezi kuwaacha nyuma, isipokuwa ni kuwapa elimu ya afya ya akili kwani wengi wao wamefanyiwa vitendo vya ukatili wa kingono na bado jamii huwaona wakosaji,” amesema na kuongeza;
“Jambo hilo kwa vyovyote linawasababishia kupatwa na msongo wa mawazo ambapo kama juhudi za ziada hazitafanyika wanaweza wasimalize masomo yao.”
Dk Khadija amesema mpaka sasa wanafanya kazi na shule sita za Wilaya ya Kinondoni ambapo malengo yao ni kutaka kuona matunda chanya katika Wilaya hiyo kwa kuja na mradi unaojulikana kwa jina la ‘Jamii Elimika’ utakaoshirikisha wanafunzi, wazazi , walimu , watoa huduma za Afya na viongozi wa dini.
Kwa upande mwingine, amesema moja ya shuguli zao pia kugawa taulo za kike, na kwamba wamebaini wengi wa wanafunzi hushindwa kwenda shule wanapokuwa katika siku zao za hedhi kutokana na kutokuwa na uwezo wa kununua bidhaa hizo.